Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Yaahidi Kuimarisha Mawasiliano Kaskazini Unguja.


Na Mwandishi wetu WMTH-Bungeni Dodoma.

Serikali imesema itahakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano, Huduma za Mawasiliano za uhakika zinawafikia wananchi wote ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kuboresha huduma za kijamii.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb) wakati akijibu swali la Mhe. Tamima Haji Abbas, Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kufahamu Mpango wa Serikali wa kuimarisha Mawasiliano ya Simu katika Vijiji vilivyopo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

Mhe. Dkt. Mkama alieleza kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), katika mwaka wa fedha 2021/2022, serikali ilitekeleza mradi wa kimkakati wa kupanua huduma za mawasiliano katika shehia 38 zilizokuwa na changamoto kubwa ya mtandao.  

Katika utekelezaji wa mradi huo, jumla ya minara 42 ya mawasiliano ikijengwa kupitia Kampuni ya Honora Tanzania (YAS) ili kuimarisha upatikanaji wa mtandao wa simu na intaneti. Ujenzi wa minara hiyo umeongeza uwezo wa wananchi kuwasiliana na pia kupata huduma mbalimbali za kidijitali.

“Kati ya Minara hiyo, Mkoa wa Kaskazini Unguja ulinufaika kwa kujengewa Minara 12 ambapo mradi huu ulikamilika na kwa sasa Wananchi wananufaika na Huduma za Mawasiliano”, alieleza Mhe. Dkt. Mkama.

Naibu Waziri Mkama aliongeza kuwa, Serikali pia imebaini uwepo wa Changamoto katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika Shehia za Mafufuni iliyoko Wilaya ya Kaskazini B na Tazari iliyopo ya Kaskazini A ambako huduma za mawasiliano bado hazijafikia kiwango kinachoridhisha. Baada ya kubaini changamoto hiyo, Serikali kupitia Mradi wa Minara 201 imempatia Kampuni ya Honora Tanzania kujenga Mnara katika Shehia ya Mafufuni.

Serikali imeahidi kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na za uhakika. Jitihada hizi zinatarajiwa kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.