Habari
SERIKALI YAAHIDI KUBORESHA MAWASILIANO MIPAKANI

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Kyela – Mbeya
Serikali imeahidi kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika katika vijiji vilivyopo mipakani ili wananchi waweze kuwasiliana na kufurahia fursa mbalimbali zinazoletwa na huduma za mawasiliano hususan katika shughuli za uzalishaji na kijamii ili kukuza uchumi na usalama wa jamii husika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, ametoa ahadi hiyo leo Oktoba 13, 2025 alipozuru katika vijiji vya Kata za Katumbasongwe, Njisi, na Ngana vilivyopo mpakani mwa Tanzania na Malawi, pamoja na Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Kasumulu kilichopo wilayani Kyela, mkoani Mbeya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Katika ziara hiyo, wananchi walieleza kuwa katika baadhi ya maeneo bado kuna muingiliano wa mawasiliano na nchi jirani ya Malawi licha ya kuwepo kwa minara ya mawasiliano bado nguvu ya mitandao hiyo imeendelea kuwa dhaifu, kutokana na jiografia ya mabonde katika maeneo hayo na kuzuia upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano.
Bw. Abdulla ameielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na kampuni za simu zinazotoa huduma katika maeneo hayo ili kufanya tathmini ya kina na kubaini suluhisho la kudumu, ikiwemo kujenga au kuongeza nguvu ya minara ya mawasiliano iliyopo.
Kwa upande wake, Nassib Kalombola, Kaimu Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Mbeya, ameipongeza Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuwezesha huduma bora za mawasiliano katika kituo cha mpaka wa Kasumulu, hatua iliyosaidia kuimarisha utendaji na ufanisi wa shughuli za forodha katika mpaka huo.
Awali, akitoa taarifa ya hali ya mawasiliano mkoani Mbeya, Meneja wa TCRA, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Bartholomew Titus, alisema hadi kufikia Juni 2025, mkoa wa Mbeya una jumla ya minara 386 ya simu na zaidi ya laini za simu milioni 5.3, huku matukio ya ulaghai wa mitandao yakipungua kutoka 1,000 hadi 803.