Habari
SERIKALI YA TANZANIA YAJIFUNZA TOKYO KUKUZA KAMPUNI CHANGA NA UBUNIFU
Na Mwandishi Wetu, WMTH, Tokyo
Ujumbe wa wataalam kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania upo nchini Japani kwa ziara ya katika Kituo cha Ubunifu cha Tokyo, kinachojulikana kama Tokyo Innovation Base (TIB), kwa lengo la kujifunza mbinu bora zinazotumika katika kuendeleza na kukuza kampuni changa (startups).
TIB ni kituo kilichoanzishwa mwaka 2023 na Serikali ya Mji wa Tokyo, kama sehemu ya mkakati wa kuifanya Tokyo kuwa kitovu cha kimataifa cha ubunifu na teknolojia.
Aidha, Kituo hiki kinahudumia wajasiriamali, kampuni changa, na wabunifu kwa kutoa huduma za ushauri, nafasi za ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, mafunzo ya kiufundi, pamoja na fursa za uwekezaji. Kwa sasa, TIB ni moja ya vituo vinavyotambulika duniani kwa kuendesha programu za kimataifa za kukuza ubunifu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo tarehe 08 Oktoba, 2025, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku, alisema kuwa wataalam hao wamefika katika Kituo cha TIB kujifunza mifumo bora ya usimamizi na uendeshaji wa vituo vya ubunifu ili kuhakikisha uendelevu na tija ya muda mrefu. “Tunataka kuhakikisha kuwa vituo vya ubunifu vinavyoanzishwa nchini vinakuwa na miundombinu imara, mifumo endelevu, na ushirikiano thabiti kati ya wadau wote,” alisema Bw. Munaku.
Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya TEHAMA inaendelea na ujenzi wa vituo nane vya ubunifu (Innovation Zones) vitakavyowezesha wabunifu na kampuni changa kukutana, kushirikiana, na kubuni suluhisho za kiteknolojia zitakazochochea uchumi wa kidijitali.
Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo umejumuisha wataalam kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tume ya TEHAMA, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).
Kupitia ziara hii, Tanzania inatarajia kuimarisha ushirikiano na Japani katika kukuza mazingira wezeshi ya ubunifu, kuongeza ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, na kuboresha mifumo ya uendeshaji wa vituo vya ubunifu nchini.
