Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI NA MPANGO WA KUHAMISHIA SHUGHULI ZOTE ZA MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO KWA TTCL


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye(Mb) akimkabidhi cheti na nyaraka za michoro Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga (kushoto) inayoonyesha jinsi na namna miundombinu ya Mkongo wa Taifa ulivyojengwa kutoka Mangaka-Mtambaswala (kilomita 72) na Arusha-Namanga (kilomita 105) ili kuliwezesha shirika kusimamia na kuendesha Mkongo huo 

 

DODOMA
 

Serikali ipo katika mchakato wa kuhamishia shughuli zote za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambapo kwa sasa Shirika hilo linajihusisha na shughuli za uendeshaji na usimamizi wa Mkongo huo na shughuli nyingine zipo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye katika kikao kazi na wakandarasi wajenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine alikabidhi vyeti vya kukamilisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa kwa zabuni za mwaka 2020/21 kwa kampuni ya Raddy Fiber Ltd, Telecom Associate, TTCL na Huawei Tanzania.

“Kama nilivyozungumza Bungeni wakati wa wasilisho la hotuba ya Bajeti ya Wizara hii Mei 20, 2022 kuwa tupo katika mchakato wa kuhamishia shughuli zote za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Shirika letu la TTCL, Wizara imeulea mpaka umekuwa na sasa upo tayari kukabidhiwa kwa Shirika hilo”, Amezungumza Waziri Nape

Ameongeza kuwa, hana mashaka na uwezo wa Mkurugenzi wa Shirika la TTCL Mhandisi Peter Ulanga katika kusimamia shughuli zote za Mkongo na ana matumaini makubwa kuwa ataweza kubeba jukumu hilo pindi mchakato wa utakapokamilika kuukabidhi kwa Shirika hilo utakapokamilika

Aidha, katika kikao kazi hicho na wakandarasi Shirika la TTCL limekabidhiwa nyaraka zenye michoro ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliokamilika ambazo ni kilomita 72 kutoka Mangaka-Mtambaswala kilomita 105 za Arusha-Namanga kwa ajili ya kuliwezesha shirika kusimamia na kuendesha Mkongo huo wakati mchakato wa kuhamishia shughuli zote za Mkongo kwa Shirika hilo Ukiendelea