Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUVUTIA WAWEKEZAJI KUKUZA UCHUMI WA KIDIJITALI


Na Juma Wange.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema Serikali inaendelea kuvutia wawekezaji ili kuwa na mikongo mingi na kushusha gharama za matumizi ya Intaneti.

Ameyasema hayo leo tarehe 05 Februari, 2024 wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyowasilishwa Bungeni jijini Dodoma.

Mhe. Mhandisi Kundo amesema safari ya Tanzania kuelekea Uchumi wa Kidigitali inahitaji miundombinu ya kidigitali ambayo ni ujenzi wa mikongo ukiwemo Mkongo wa Baharini, Mkongo wa Taifa na mkongo wa watumiaji wa mwisho inayohusisha minara pamoja na fibre mlangoni kwako. 

Amesema kuwa, Mhe. Rais alipoingia madarakani alitoa kiasi cha shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unajengwa na kufika katika wilaya nyingi zaidi.

Sambamba na hilo, Mhe. Mhandisi Kundo amewaeleza wabunge kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha kiasi cha dola za kimarekani milioni sita  kwa ajili ya ujenzi wa ICT Hubs katika Mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Lindi, Mwanza, Arusha na Zanzibar. 

"Lengo ni kuwaandaa vijana wawe tayari kuingia katika soko la kidigitali ili Tanzania yetu iingie katika Uchumi wa Kidigitali,” amesema Mhe. Mhandisi Kundo. 

Ameongeza kuwa, katika teknolojia zinazoibukia, tayari Serikali imeandaa miongozo mbalimbali na sera ili kuhakikisha kwamba tunajilinda dhidi ya majanga ya kimtandao.