Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUTATHMINI UPYA UTENDAJI WA BARAZA LA USHAURI LA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO


Serikali imeamua kutathimini upya utendaji wa Baraza la Ushauri la Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC) kutokana na kutoridhishwa na uhusiano uliopo kati ya watoa huduma na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini. Serikali pia imesimamisha kupanda kwa gharama za bando hadi tathmini ya gharama za mawasiliano inayoendelea itakapokamilika. Tathmini ya mwisho ilifanyika mwaka 2018.

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA-CCC) lilianzishwa chini ya kifungu cha 37 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003. Kuanzishwa kwa TCRA-CCC kulilenga kulinda haki na maslahi ya watumiaji wa bidhaa na huduma za mawasiliano katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Utangazaji na Huduma za Posta.

Kuanzishwa kwa Baraza hili kulikusudiwa kuwa na lengo la kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasilisho nchini, kutoa maoni na taarifa pamoja na kushauriana na TCRA, Mawaziri wa Sekta, kupokea na kusambaza taarifa na maoni juu ya masuala yenye maslahi kwa watumiaji wa bidhaa na huduma za mawasiliano, kushauriana na wadau wa Sekta ya Mawasiliano, Serikali na vikundi vingine vya watumiaji juu ya maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano katika mambo kadhaa, ikiwemo suala la huduma za intaneti za bando. Sambamba na kupokea na kuwasilisha malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano Baraza lina wajibu wa kutoa elimu juu ya suala la huduma za intaneti za bando kwa umma pamoja na mambo mengine yanayohusiana na watumiaji wa huduma za mawasiliano.

Baraza linapaswa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za huduma za mawasiliano ikiwemo suala la gharama za intaneti za bando kama ambavyo limekuwa likiwatatiza watumiaji siku za karibuni.

Kwa kuwa Bodi ya Baraza iliyopo imemaliza muda wake, na kwa kuwa Serikali ina lengo la kuhakikisha majukumu ya Baraza hayakwami na yanaboreshwa, Mheshimiwa Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amwemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akamilishe mchakato mara moja wa kuunda Bodi mpya ya Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano. Serikali inaongeza siku saba za za kupokea maombi ya wanaotaka kuhudumu kwenye Baraza hilo. Serikali itaendelea kupokea maombi hadi tarehe 28 Novemba 2022.

Baada ya kupatikana kwa Bodi ya Baraza hilo, tunatarajia itafanya kazi zake kwa ufanisi ikiwa ni kamoja na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu huduma za mawasiliano nchini. Maoni yatakayokusanywa na Baraza yatasaidia kuboresha mahusiano yaliyopo kati ya watoa huduma na watumiaji wa huduma za mawasiliano na Serikali pia itafanya marekebisho ya kutunga kanuni za kuboresha utendaji wa kazi za Baraza.

Aidha, Serikali inaielekeza Mamlaka ya Mawasiliano nchini kuwezesha Baraza hili na kuhakikisha linapata bajeti ya kutosha kufanya shughuli zake zinazojumuisha za kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala yote yanayohusu maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini. Serikali itahakikisha Baraza linapata fedha za kutosha kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Nia ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha taasisi zake zinafanya kazi kwa ufanisi na kuwahudumia Watanzania kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa kupitia maelekezo ya kisera.