Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUSHUGHULIKIA MTAJI WA BILIONI 20.9 KWA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kushughulikia maombi ya mtaji wa Shirika la Posta Tanzania ili kuliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake kuendana na lengo la uanzishwaji wa Shirika kwa mujibu wa Sheria iliyounda Shirika hilo.

Hayo yameelezwa leo tarehe 03 Agosti, 2022 na Msajili wa Hazina Ndg. Mgonya Benedicto wakati akifungua Kikao Kazi cha Viongozi wa Shirika la Posta Tanzania katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu SUA, Mjini Morogoro.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Ndg. Mgonya ameeleza kuwa Serikali kwa kutambua mchango wa Shirika la Posta hasa katika Sekta ya Mawasiliano nchini inaendelea kushughulikia suala la kulipa Shirika hilo mtaji wa Bilioni 20.9, lengo likiwa ni kulitengenezea mazingira wezeshi Shirika la Posta katika kutimiza majukumu yake.

Aidha, Ndg. Mgonya ameongeza kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewasilisha mapendekezo ya maombi ya mtaji wa Shilingi bilioni 20.9 kwa Wizara ya Fedha na Mipango na kuahidi kuendelea kufuatilia suala hilo kwa utekelezaji wa haraka ili kulifanya Shirika liendelee kutoa huduma stahiki na zinazoendana na mahitaji ya wakati ya wananchi.

“Nazifahamu changamoto mlizonazo ikiwemo maombi ya mtaji wa Shilingi bilioni 20.9, na niwahakikishie kupitia Mkutano huu, Ofisi ya Msajili wa Hazina kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tumezibeba changamoto hizi, mbali na kuwasilisha maandiko haya Wizara ya Fedha na Mipango, tunaendelea na ufuatiliaji na tuna imani kuwa changamoto zote hizi zitafanyiwa kazi”. Amesema Ndg. Mgonya 

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kupitia ofisi ya Msajili wa Hazina Ndg. Mgonya Benedicto kwa kuendelea kulitengenezea Shirika mazingira wezeshi huku akielezea mipango ya Shirika katika kuendelea kuboresha huduma zake kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wa 8 wa kibiashara wa Shirika kwa miaka minne (2022/23 - 2025/26) wenye dhumuni ya kuifanya Posta ya Kidijitali kwa biashara endelevu (Digitalization of Post for Business Improvement and Sustainability) lengo ikiwa ni kutoa huduma stahiki na zenye ubora kuendana na vionjo vya wateja 

“Ili kuendana na vionjo vya wateja wetu vilivyobadilika na pamoja na kuendana na dira ya Taifa tumedhamiria kuifanya Posta ya Kidijitali kupitia mpango mkakati wetu wa 8 wa biashara wa Shirika ili kila mwananchi anufaike na huduma zetu”. Amesema Bw. Mbodo 

Kikao hicho kilichowakutanisha viongozi wote wa Shirika la Posta kuanzia ngazi ya mikoa, Zanzibar na Makao Makuu kina lengo la kutathmini utendaji kazi wa Shirika kwa kipindi kilichopita cha mwaka wa fedha 2021/22 pamoja na kuangalia namna ya kutatua changamoto zilizojitokeza kwa kipindi cha mwaka huo uliopita na pia kusainiana malengo ya mwaka wa fedha 2022/2023.