Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUONGEZA NGUVU KUKABILIANA NA MUINGILIANO WA MAWASILIANO YA MIPAKANI


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Bungeni, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habati imesema inaendelea kuongeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano maeneo ya mipakani ili kupunguza changamoto ya muingiliano wa mawasiliano, sambamba na ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya Reli ya Kisasa (SGR) na barabara kuu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), leo Februari 02, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara.

Mbunge huyo alihoji kuhusu changamoto ya muingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani, pamoja na udhaifu wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Hifadhi ya Serengeti na vijijini kwa ujumla.

Akijibu swali hilo, Waziri Kairuki amesema Serikali inatambua changamoto ya udhaifu wa mawasiliano, hasa katika maeneo ya mipakani ikiwemo Sirari, Tarime na maeneo mengine yanayopakana na nchi jirani.

Ameeleza kuwa katika Awamu ya Kumi na Moja, maeneo hayo yamepewa kipaumbele maalum, ikiwemo maeneo yanayopitiwa na reli ya SGR pamoja na barabara Kuu.

Aidha, Waziri Kairuki amebainisha kuwa Serikali tayari imechukua hatua mbalimbali za kupunguza na kuondoa muingiliano wa mawasiliano, na itaendelea kuchukua hatua zaidi licha ya changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika maeneo ya mipakani.