Habari
Serikali Kumaliza Changamoto za Mawasiliano Nchini Ifikapo 2030
Na Mwandishi Wetu WMTH, Bungeni-Dodoma.
Serikali imeeleza dhamira yake ya kumaliza kabisa changamoto za huduma za mawasiliano nchini ifikapo mwaka 2030 kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa 2025–2030 unaotekelezwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 25, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Paul Mnzava, kuhusu lini Serikali itatatua changamoto ya ukosefu wa huduma za mawasiliano ya simu katika Kata ya Kalalani.
Naibu Waziri Mkama amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) tayari imefanya tathmini ya hali ya mawasiliano katika vijiji vya Mtoni Bombo na Kalalani. Amesema kijiji cha Mtoni Bombo kimebainika kuwa na changamoto kubwa ya huduma za mawasiliano, huku kijiji cha Kalalani, licha ya kuwa na minara miwili inayohudumiwa na kampuni tatu za simu, bado kinakabiliwa na changamoto ya huduma duni kutokana na ukubwa wa eneo hilo na shughuli nyingi za kiuchumi, ikiwemo uchimbaji wa madini.
Aidha, Serikali kupitia UCSAF imeahidi kujumuisha vijiji vya Mtoni Bombo na Kalalani katika bajeti ya ujenzi wa minara ya mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Akijibu swali la nyongeza kuhusu kuharakishwa kwa utatuzi wa changamoto hiyo, Mhe. Dkt. Mkama ameielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya tathmini ya kina ya huduma za mawasiliano katika kata hiyo, sambamba na kuwataka watoa huduma za simu kuongeza nguvu ya minara iliyopo ili kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
