Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUENDELEA KULIWEZESHA JESHI LA POLISI KUBORESHA UTENDAJI KAZI


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

 

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania na kuliwezesha kwa vifaa vya kisasa vya mawasiliano na teknolojia ili kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kimtandao nchini.

 

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa na Uzinduzi wa Maabara ya Uchunguzi wa Makosa ya Kimtandao iliyofanyika leo tarehe 19 Juni 2026 katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Abdulla amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA na usalama wa kimtandao kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo kuwajengea uwezo wataalamu pamoja na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za uchunguzi wa makosa ya kimtandao.

 

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinakuwa na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mbinu mpya za uhalifu wa kimtandao zinazojitokeza katika mazingira ya kidijitali.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Ally Senga Gugu amepongeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuendelea kuimarisha usalama wa kimtandao ndani ya Jeshi la Polisi, akibainisha kuwa ujio wa vifaa hivyo utaongeza ufanisi katika uchunguzi wa makosa ya kimtandao na kuimarisha usalama wa nchi dhidi ya vitendo vya uhalifu vinavyotumia teknolojia za kidijitali.

 

Aidha, amesema hatua hiyo itaifanya Tanzania kuwa salama zaidi na imara katika kukabiliana na changamoto za uhalifu wa kimtandao, huku ikiimarisha uwezo wa vyombo vya dola katika kulinda wananchi na mali zao.