Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KULINDA MASLAHI YA WANAHABARI


MWANZA

Serikali imesema imedhamiria kulinda maslahi ya waandishi  wa habari nchini kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakakabili.

Hayo yamesemwa  na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye , jijini Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana wakati aliposhiriki katika tukio  la kuaga miili ya wanahabari 5 waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea jana  Januari 11, 2022 katika Wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu wakati wakielekea kwenye ziara ya kukagua miradi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel

Mhe. Nape amewataka waajiri wa waandishi wa habari waliopata ajali na kufariki katika ajali hiyo kuwalipa maslahi yao kwa familia za marehemu.

"Natoa siku 7 kwa waajiri wote  kuanzia leo kulipa haki za wanahabari waliofariki na taarifa za uthibitisho wa malipo iwasilishwe kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza" alisisitiza Waziri Nape

Aidha, Waziri alisema kuwa Serikali itapitia upya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo ili kuboresha maslahi ya Wanahabari nchini.

"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza tupitie mapungufu ya sheria hiyo na kurekebisha ,  mimi nitahakikisha  nalinda uhuru na haki zenu ziko salama mikononi mwa Rais Samia, nami nitasimamia kwa kuwa sasa nimerudi nyumbani kusimamia sheria hii na tutahakikisha haki zenu zinalindwa kwa vile mimi ni muasisi wa sheria hii" Alisisitiza Waziri Nape

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Mhe. Mhandisi Gabriel alisema kuwa huu umekua msiba wa Taifa na Viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan  wametuma salamu za pole kwa wafiwa na wananchi wa Mkoa wa Mwanza.

Aidha, aliongeza kuwa Mkoa wa Mwanza umepata pigo kubwa na watahakikisha viongozi wa Mkoa huo wanaendelea  kutoa ushirikiano kwa wanahabari nchini ili kusaidia waendelee kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Wanahabari  watano waliofariki katika ajali hiyo ni Abel Ngapemba, Afisa habari wa Mkoa wa Mwanza, Steven Masengi, Afisa habari Wilaya ya Ukerewe na Husna Milanzi mwandishi wa ITV, Johari Shani mwandishi wa Uhuru digital na Anthony Chuwa mwandishi wa kujitegemea.

 

.