Habari
SERIKALI KUJENGA MINARA 15 YA MAWASILIANO MANYONI
Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema Serikali inatarajia kujenga jumla ya minara 15 katika kata mbalimbali za Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Naibu Waziri Maryprisca amesema hayo tarehe 13 Mei, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Isseke, Wilaya ya Manyoni akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa mnara wa mawasiliano unaojengwa na kampuni ya simu ya Airtel kwa kushirikiana na UCSAF.
Amesema minara hiyo 15 itajengwa katika kata za Isseke, Makanda, Makutupora, Maweni, Mitundu, Mkwese, Mwamagembe, Nkonko, Rungwa, Sanjaranda, Sanza, Saranda, Sasajila na Sasilo ili kuimarisha huduma za mawasiliano.
Akizungumzia Mnara wa Isseke unaoendelea na ujenzi, Mhandisi Maryprisca amesema umeigharimu Serikali jumla ya Tsh. 116,500,000/- ambapo asilimia 70 ya fedha hizo ambazo ni Tsh. 81,550,000/- tayari zimeshalipwa na UCSAF kwa Airtel.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa mnara huo na kuanza kutoa huduma ya Mawasiliano kutawasaidia wakazi wa Vijiji vitakavyofikiwa kwa kuboresha shughuli za kiuchumi na kupata mawasiliano kwa haraka hususan taarifa muhimu za masoko.
Amesema mawasiliano ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Manyoni kwani yatasaidia pia kuokoa muda wa kufunga safari ili kupata huduma umbali mrefu na kurahisisha huduma za kutuma na kupokea pesa ambazo sasa zitafanyika majumbani.
"Tunaishukuru sana kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kushirikiana na UCSAF, kwa kuchukua uamuzi huu wa kuipa Wilaya ya Manyoni kipaumbele na kuamua kufikisha huduma za mawasiliano ya uhakika kwa wakazi zaidi ya 6,900 wa vijiji zaidi ya vinne wilayani hapa vikiwemo Igwamadete, Mpapa, Simbunguru na Isseke yenyewe," alisema Mhandisi Maryprisca.
Katika hatua nyingine Mhandisi Maryprisca amewahimiza wananchi wa Manyoni kuhakiki Anwani zao za makazi kwa kuwa Mfumo wake umeendelea kuboreshwa ambapo tarehe 16 Aprili, 2024 wizara ilizindua majaribio ya Utoaji wa barua ya Utambulisho wa Ukaazi kwa njia ya kidijitali bila hitaji la Mwananchi kwenda kwenye Ofisi za Serikali ya Mitaa.
"Unaweza kupata barua husika kupitia simu yako ya kiganjani ukiwa mahali popote hivyo nawakumbusha kuhakiki Anwani zenu kwa kutumia huduma hii inayowaondolea usumbufu na kupunguza muda wa kupata huduma hii," alisisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Bw. Pius Joseph akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa UCSAF amewaeleza Wananchi wa Isseke kuwa upanuzi wa huduma za mawasiliano katika kata hiyo ni kati ya mikakati waliyojiwekea UCSAF kwa kushirikiana na kampuni za simu za mkononi kwa kutambua umuhimu wa huduma za mawasiliano hasa maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake Mhe. Dr. Pius Chanya (Mb) wa Manyoni Mashariki ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Habari kwa kuendelea kuwapelekea miradi ya maendeleo wananchi wa Manyoni jambo linalowawezesha kukua kiuchumi.