Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Kuimarisha Mawasiliano Katika Maeneo ya Kimkakati Nchini


Na Mwandishi Wetu, WMTH

Bungeni, Dodoma

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika maeneo yote ya kimkakati nchini ili kuimarisha huduma za mawasiliano, ikiwemo maeneo ya hifadhi za wanyama, reli ya kisasa ya SGR, reli ya TAZARA pamoja na barabara kuu.

 

Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo Mei 25, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi katika kipindi cha maswali na majibu kuhusu upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kufuatia maswali yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu sekta hiyo.

 

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa minara ya mawasiliano nchini kwa lengo la kupunguza changamoto za huduma hiyo, hususan katika maeneo muhimu ya kiuchumi na kijamii.

 

“Tunatekeleza miradi minne ya ujenzi wa minara ya mawasiliano ambapo mradi wa minara 758 tayari umekamilika. Mkoa wa Tanga umefanikiwa kupata zaidi ya minara 43. Aidha, kuna miradi mingine ya minara 636 na 201 inayotarajiwa kukamilika mwaka ujao,” amesema Waziri Kairuki.

 

Ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za mawasiliano katika Mkoa wa Tanga na maeneo mengine nchini, huku akisisitiza kuwa Mkoa wa Tanga una umuhimu mkubwa kiuchumi na kimkakati kutokana na shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na kuwa mkoa wa mpakani.