Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUFIKISHA HUDUMA YA INTANETI, SIMU NYUMBA ZA TEMBE


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka wakisaini mkataba wa ushirikiano baina ya Wizara hiyo na TANESCO ya ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kutumia miundombinu ya umeme, Dar es Salaam. Wanaoshuhudia nyuma wa kwanza katikati ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile na kulia kwake ni Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani.

  • Kujenga Kilomita 4,244 badala ya 1,880 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
  • Yatenga Shilingi Bilioni 170 kwa Ujenzi Huo katika mwaka 2021/2022
  • Kutumia Miundombinu ya TANESCO kufikisha Intaneti, Simu kwa Wananchi

 

Na Prisca Ulomi, WMTH

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetiliana saini leo ya mkataba wa ushirikiano na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ya ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kutumia miundombinu ya umeme ili kuongeza kasi ya ufikishaji wa huduma ya intaneti, simu na televisheni kwa wananchi

Utiaji saini wa mkataba huo umefanywa na Katibu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka kwenye ofisi ya Mkoa wa Ilala, TANESCO, Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani

Dkt. Ndugulile asema kuwa lengo la utiaji saini wa ushirikiano baina ya Wizara yake na TANESCO ni kuhakikisha kuwa Serikali inaongeza maeneo na ushirikiano yatakayopelekea kuongeza tija, kasi ya ufikishaji wa miundombinu ya mawasiliano na usambazaji wa umeme nchini pamoja na kupunguza gharama za ujenzi wa miundombinu hiyo ili palipo na nguzo ya umeme kuwepo na huduma ya intaneti, simu na televisheni kwa kuwa tayari Serikali imefikisha huduma za umeme kwa wananchi mpaka kwenye nyumba za tembe

Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 170 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 1,880 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo kwa kutumia miundombinu ya umeme ujenzi wa kilomita hizo utaongezeka na kufikia kilomita 4,244 hivyo kuiwezesha Serikali kuwa na jumla ya kilomita 12,563 ifikapo mwaka 2022 kwa kuwa hivi sasa tayari kuna kilomita 8,913 za Mkongo huo

Naye Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa utiaji saini wa mkataba huu leo ni matunda na matokeo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Wizara zizungumze na hii ni dalili njema kwa kuwa wote ni Serikali na tunamhudumia mwananchi huyo huyo na hakuna tofauti baina ya nguzo za umeme na nguzo za mawasiliano za TTCL hivyo kwa wananchi hii tofauti ya miundombinu ya nguzo haipo

Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa mkataba huo utatoa fursa mpya kwa Wizara kutumia miundombinu ya mawasiliano iliyojengwa na TANESCO kufikisha huduma za mawasiliano mpaka nyumbani kwa mwananchi; na TANESCO kutumia miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano itakayojengwa kufikisha umeme kwa wananchi kwenye makazi yao hivyo kupunguza gharama za ujenzi wa miundombinu hiyo kwa kutumia mkataba huu  na Wizara itashirikiana na TANESCO ili malengo na maslahi ya Taifa yaliyowekwa yaweze kufikiwa kwa wakati

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameupongeza uongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na TANESCO kwa kusaini mkataba huo kwa kuwa Serikali itakuwa imewasaidia wananchi kupata huduma za mawasiliano na umeme na ametoa rai kwa watendaji wahakikishe utekelezaji wa mkataba huu unafanyika kikamilifu na waendelee kutumia mawazo ya wazee wazalendo wa TANESCO na TTCL kwa kuwa wana utaalam na wanazeeka umri bali mawazo yao bado yako pale pale

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema kuwa mkataba huo utawezesha matumizi na uwekezaji mpya kwenye miundombinu ya mawasiliano ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na ya umeme ya TANESCO ambapo itaongeza kasi ya kuwafikia wananchi kwa kuwa tutakuwa tumefikisha umeme na mawasiliano kwa mwananchi kwa wakati mmoja hivyo Serikali itakua imeua ndege wawili kwa wakati mmoja

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi akitoa salamu za shukrani baada ya utiaji saini wa mkataba huo amesema kuwa Serikali ni moja na ndiyo inayotoa fedha za kujenga miundombinu hii na inalenga kumhudumia mwananchi huyo huyo hivyo ni jambo jema kwa taasisi za Serikali kushirikiana kwa kuwa mwananchi atapata huduma zote tatu kwa wakati mmoja ikiwemo intaneti, simu na televisheni

Utiaji saini huo umeshuhudiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Henry Mahimbali; Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa; Wakuu wa taasisi wa TTCL, Shirika la Posta Tanzania; Menejimenti na watendaji wa Wizara mbili tajwa hapo juu