Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUFANYA TATHMINI YA UPATIKANAJI NA UBORA WA MAWASILIANO


Na Faraja Mpina.

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imepanga kufanya tathmini ya hali ya upatikanaji na ubora wa huduma za mawasiliano katika kata za majimbo ya Wingwi, Ukerewe, Konde, Kilindi na Morogoro Kusini Mashariki. 

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew leo Februari 2, 2024 Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Omar Issa Kombo Mbunge wa Wingwi, na maswali ya nyongeza yaliyoulizwa na Mhe. Furaha Matondo (ukerewe); Mhe. Mohammed said (Konde); Mhe. Shabani Taletale (Morogoro Kusini Mashariki); Mhe. Omari Kigua (Kilindi) yote yakihusu changamoto za huduma ya mawasiliano katika baadhi ya kata za majimbo hayo. 

Mhandisi Kundo akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye amesema kuwa, tayari Serikali imeshafanya tathmini katika vijiji 2116 na kupandisha hadhi minara 304 iliyokuwa inatumia teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G; 

Katika hatua nyingine, Mhandisi Kundo ameelezea mpango wa Serikali wa kujenga minara 636 ambayo itaenda kutatua changamoto za mawasiliano katika maeneo ambayo hayakuwekwa kwenye mpango wa minara 758 inayoendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amewaelekeza wataalamu wa Wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi zake za UCSAF na TCRA kwenda kufanya tathmini mara moja ili kujiridhisha  hali ya upatikanaji wa huduma katika maeneo ambayo wabunge wameyataja kwa lengo la  kuona hatua gani zinachukuliwa kutokana na majibu watakayoyaleta.

Pamoja na hilo amefafanua kuwa mnara wa mawasiliano wa TTCL unajengwa katika kata ya Sizini kwa ufadhili wa UCSAF awamu ya sita na unatarajia kukamilika na kuwashwa mwezi Aprili 2024, na minara yenye teknolojia ya 2G itaendelea kupandishwa hadhi kwenda 3G na 4G kwa kadiri fedha zitakavyokuwa zinapatikana.