Habari
SERIKALI KUENDELEZA JITIHADA ZA KUHAKIKISHA MIFUMO YA SERIKALI INASOMANA
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeahidi kuwa itahakikisha mifumo yote ya Serikali inasomana, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kuondoa usumbufu unaotokana na urasimu wa mifumo isiyounganishwa.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 9 Februari, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Waziri Kairuki amesema juhudi hizo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu umuhimu wa mifumo ya Serikali kufanya kazi kwa pamoja ili kumpunguzia mwananchi gharama, muda na usumbufu katika kupata huduma mbalimbali.
Ameongeza kuwa Wizara inaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA kwa kushirikiana na taasisi na wizara nyingine ili kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa urahisi, kwa usalama na kwa ufanisi mkubwa, sambamba na kulinda taarifa za wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Selemani Kakoso, ameipongeza Wizara kwa uwasilishaji wake na kuishauri Serikali kuhakikisha mapendekezo yote yaliyotolewa yanafanyiwa kazi kwa haraka ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Kakoso amesema utekelezaji wa mapendekezo hayo utasaidia kuongeza uwajibikaji wa taasisi za Serikali na kuchochea matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma mbalimbali nchini.
