Habari
Serikali Itaendelea Kuweka Mazingira Bora kwa Uwekezaji wa Huduma za Mawasiliano.
Na Mwandishi Wetu, WMTH-Dar es Salaam.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ametembelea Kampuni ya YAS Tanzania katika ziara yake ya kikazi iliyofanyika leo katika ofisi za makao makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki ameipongeza YAS Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kuchochea mapinduzi ya kidijitali nchini, hususan katika miamala ya kifedha, upanuzi wa mawasiliano vijijini, uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, pamoja na ajira wanazozitoa kwa Watanzania.
Aidha, Waziri Kairuki ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwekeza kiasi cha USD milioni 47.6 katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ndani ya kipindi cha miaka mitatu, sambamba na ushirikiano wake na Serikali katika ujenzi wa minara 560 ya mawasiliano na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Amesema Kampuni ya YAS ina wajibu wa kuendelea kuwaunganisha wananchi na huduma za mawasiliano, hasa wale wanaoishi vijijini, bila kumwacha mtu yeyote nyuma — wakiwemo wanawake, watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo pembezoni.
Pia, Waziri Kairuki ameitaka Kampuni ya YAS kuongeza uwekezaji katika miamala ya kifedha na kuhakikisha inalinda faragha na usalama wa taarifa za wateja wake. Ameihimiza kampuni hiyo kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma wanazotoa, pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wake kupitia mafunzo ya mara kwa mara ili waendane na mabadiliko ya teknolojia.
Waziri Kairuki ameipongeza YAS kwa kutoa mafunzo kwa vijana takribani 9,000, na ameitaka kuongeza juhudi katika kuwawezesha vijana hasa wasichana kwa ujuzi wa TEHAMA.
“Kwa upande wetu, tutaendelea kujenga mazingira wezeshi ili muweze kuona matunda ya vijana mnaowawezesha kupitia mafunzo haya,” alisema Waziri Kairuki.
Aidha, Waziri Kairuki amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuandaa sera zinazowezesha kampuni kama YAS kukua kibiashara, kulinda maslahi ya watumiaji na kuimarisha uchumi wa taifa. Ameongeza kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na kampuni hiyo kuwekeza katika maeneo ya kimkakati, yakiwemo maeneo ya utalii kama visiwa, pamoja na maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara.
Akihitimisha, Waziri Kairuki aliishukuru YAS Tanzania kwa ushirikiano wake na kusisitiza kuwa kuendelea kuimarisha mahusiano hayo kutaiwezesha nchi kujenga jamii jumuishi, yenye huduma salama, za kisasa na zenye ushindani kwa mustakabali wa maendeleo ya kidijitali ya Tanzania.
