Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI INATAMBUA, KUKUBALI  NA KUTATUA HOJA SEKTA YA HABARI: WAZIRI NAPE


 

Na Paschal Dotto-WHMTH.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka wanahabari kushirikiana na Kamati iliyoundwa ili kwenda kuangalia uchumi wa Vyombo vya Habari na Wanahabari wenyewe ili waweze kutatua na kuifanya sekta ya Habari kuwa bora zaidi.

Akizungumza na Wafanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Mwananchi, Waziri Nape amewataka Mwananchi kutumia vyombo vyao vya Habari kuhamasisha wanahabari kutoa ushirikiano ikiwa watafikiwa na Kamati hiyo ambayo inafanya kazi kwa muda wa miezi mitatu na kuwasilisha ripoti kwa Serikali kuhusu uchumi wa vyombo vya Habari kama Rais Samia Suluhu Hassan alivyoaagiza.

“Michakato ya mambo mbalimbali ambayo tunaendelea nayo tunategemea ushiriki.    mkubwa kwenu wanahabari hasa ushiriki maalum kutoka gazeti la mwananchi kuwahamasisha wanahabari kushirikiana na Kamati ya Kuangalia Uchumi wa Vyombo vya Habari nchini, wanahabari toeni mapendekezo kwa kamati hiyo ili tupate namna bora zaidi ya kwenda katika tasnia hii”, Waziri Nape.

Waziri Nape alisema Serikali inatambua na kukubali hoja zote zilizoko kwenye sekta ya Habari na iko tayari kuzitatua na katika kutekeleza hayo Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016 ambao una makubaliano ya pande zote mbili yaani Serikali na Vyombo vya Habari.

“Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 umekabidhiwa Bungeni na Bunge litaukabidhi kwa Kamati husika, nina matumaini yangu kuwa mwananchi mtatusaidia kuhamisisha waandishi wa Habari kuhusu Sheria hii, wito wangu ni kwamba tuzungumze kwa Pamoja kutengeneza hili jambo kwa vizazi vijavyo”, Alisema Waziri Nape.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Limited, Bakari Machumu, ameishukuru serikali kwa kutekeleza mambo mbalimbali ikiwemo lile la ukamishaji wa Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 ambayo imefikia hatua nzuri ya utekelezaji wake.

Machumu alisema kuwa Mwananchi wamekuwa wakishirikiana na serikali katika ufanyaji kazi ikiwemo kuwajengea uwezo wa kitalaamu Maafisa Habari kutoka taasisi mablimbali, lakini pia utekelezaji wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao utatoa fursa kwa mwananchi kusambaza magazeti yake kwa maeneo mengi nchini.

“Tumekuwa tukifanyakazi kwa ushirikiano wa na Serikali hivi sasa tuna mafunzo ya Inforgraphics kwa maafisa Habari watano kutoka serikalini ambao tunawajengea uwezo wa kihabari wa utoaji taarifa”, Alisema Bakari Machumu.

Aidha, Machumu alisema kuwa kuundwa kwa Kamati ya kuangalia hali ya uchumi wa vyombo vya Habari na wanahabari ni jambo ambalo litaimarisha utendaji wa sekta ya kuongeza ari ya waandishi wa Habari kutekeleza majukumuyao.