Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI IMEANZA KUSHUGHULIKIA UDHALILISHAJI  UNAOFANYWA NA WATOA MIKOPO MTANDAONI.


NA MWANDISHI WETU, WHMTH, DODOMA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amesema Serikali imeanza kushughulikia tatizo la udhalilishaji unaofanywa kwa njia ya simu kutokana na mikopo ya mtandaoni.

 Waziri Nape amebainisha hayo leo tarehe 27 Juni, 2024, Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa maelezo baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Akson kuitaka Serikali kuangalia namna ya kuidhibiti mikopo hiyo aliyosema imekuwa ikiwakera watu wasiohusika.

"Ni kweli kwa muda sasa, kumekuwa na changamoto hii ya watu wanaokopeshana mitandaoni lakini baadaye wanatumia taarifa za wanaomzunguka yule waliyemkopesha, kwa maana ya namba za simu na kuanza 'kuharasi' pale waliposhindwa kurudisha mkopo wao," alisema Waziri Nape.

Amesema, tayari Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Kitengo cha Makosa ya Mtandao cha Jeshi la Polisi, kushughulikia changamoto hiyo.

"Ndugu Spika, tumewaagiza wenzetu wa TCRA, lakini wakishirikiana na Cyber Crime Unit cha Jeshi la Polisi, kulifanyia kazi, ni matumaini yangu hii kazi itakamilika mapema ili tuone msingi wa hili jambo, ukubwa wake, na wapi wanapozipata hizi namba" amebainisha Waziri Nape.

Amesema, msingi mkubwa wa tatizo hilo ni udhalilishaji unaofanyika baada ya kushindwa kulipana baada ya kukopeshana, kwa mtu kuchukua namba za simu za watu wengi sana, wenye uhusiano na yule waliyemkopesha.

"Tunatafuta hili jambo limetokea wapi ili tuchukue hatua na kulikomesha" alieleza Waziri Nape na kuongeza kuwa, "hili jambo si jambo la kiungwana ni kinyume cha sheria.”

Waziri Nape amesema, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, inazuia kutumia taarifa za watu wengine, kufanya chochote na hizo taarifa, na kwamba hilo jambo ni kinyume cha sheria, ni nje ya utaratibu, si la kiungwana, na linalopaswa kukomeshwa.