Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI HAIFURAHISHWI NA MAHUSIANO YA WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO  NA WATUMIAJI


Na Innocent Mungy, WHMTH, Bungeni,  DODOMA

Serikali haifurahishwi na mahusiano yaliyopo kati ya watoa huduma na watumiaji huduma za Mawasiliano nchini*

Hayo yamesemwa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (MB) wakati akichangia Mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa utakaotekelezwa Mwaka 2023/2024.

“Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu yanayoonyesha kutoridhishwa kwa watumiaji huduma na huduma wanazopewa” amesema Mhe. Nnauye.

Amesema Serikali inachukua hatua kadhaa kutatua tatizo hili na kuboresha usimamizi wa huduma za Mawasiliano nchini.

Amesema Serikali Inafanya tathimini ya kupitia upya bei halisi ya gharama za kusafirisha Data nchini. Tathimini hii hufanyika Kila miaka 5 na ilifanyika mara ya mwisho Mwaka 2018, miaka 5 iliyopita. Mwaka huu inafanyika na matokeo tutayapata Disemba 2022 na kuanza kutumika Januari 2023.

Amesema inategemewa kuwa huenda gharama zitashuka kutokana na uwekezaji kwenye miundombinu ya TEHAMA na hatua zingine kadhaa zilizofikiwa.

Pia amesema Serikali inapitia upya Kanuni zinazosimamia huduma za Mawasiliano nchini hasa eneo la wajibu wa watoa huduma, watumiaji huduma na huduma zenyewe. Mapitio haya yatazingatia maoni ya wananchi ya namna ya kuboresha huduma.

Kwa mfano matangazo ya mabadiliko ya bei hutangazwa na watoa huduma kwenye vyombo vya habari badala ya kila mtumiaji huduma kutumiwa kwenye Simu yake siku moja kabla ya mabadiliko ili mtumia huduma awe na chaguo la kuendelea kutumia huduma hizo au la.