Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SEKTA YA HABARI IMETULIA NA INAKWENDA VIZURI- WAZIRI NAPE


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameipongeza sekta ya habari nchini kwa kushiriki kikamilifu na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na elimu ya kutosha kuhusu matukio ya kitaifa na shughuli za maendeleo akitolea mfano janga la uviko 19 na zoezi la Sensa ya watu na Makazi.

Akizungumza wakati wa Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini lililofanyika Desemba 17, 2022 jijini Dar es Salaam Waziri Nape ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia kwa dhamira ya dhati ya kulinda uhuru wa habari nchini.

“Uhuru wa habari ni msingi wa furaha, amani na maendeleo katika jamii na unalindwa kwa mujibu wa sheria na sio utashi wa viongozi, tayari Serikali imefanyia kazi mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya huduma za habari na ifikapo Januari 2023 yatawasilishwa Bungeni”, amezungumza Waziri Nape.

Aidha, ametoa rai kwa wanahabari kufuata miiko na maadili ya uandishi wa habari na kutumia kalamu zao kuandika makala zinazochochea amani, furaha na maendeleo katika jamii. Ameongeza kuwa tasnia ya habari ina wajibu wa kulinda maadili, tamaduni na rasilimali za nchi.

“Niwahakikishie kuwa Wizara ninayoiongoza itaendelea kushirikiana na wanahabari pamoja na wadau wengine kuhakikisha inajenga mazingira wezeshi ya kiutendaji, kulinda maslahi ya vyombo vya habari na wanahabari pamoja na kutatua changamoto za sekta ya habari nchini”, amesisitiza Waziri Nape

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema Wizara inatambua mahitaji na haki ya wananchi kupata habari na huduma za mawasiliano hasa katika wakati huu ambao mabadiliko ya teknolojia ya TEHAMA yamebadilisha mfumo mzima wa utoaji na upokeaji wa taarifa.

 Ameongeza kuwa, kupitia Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari ambalo litakuwa endelevu litatumika kama jukwaa la kukaa pamoja na wadau wa Sekta ya Habari nchini ili kujadili namna bora ya kuimarisha na kuboresha Sekta ya Habari sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri nchini, Bw. Deodatus Balile amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeleta mabadiliko mengi katika Sekta ya Habari nchini, ikiwa ni pamoja na kufungulia magazeti yaliyofungiwa. Kupitia Kongamano hilo wanahabari watajadili mchango wa Sekta ya Habari katika kukuza uchumi wa nchi.

Mwakilishi Mkazi wa UNESCO Tanzania, Michel Toto amesema UNESCO ipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali, Asasi za kiraia na wadau wa sekta ya habari nchini ili kukuza sekta ya habari  kwa kushiriki kulinda maslahi ya wanahabari; kujenga uwezo na tafiti; utungaji wa sera; kuhamasisha usawa, demokrasia na haki za binadamu katika kukuza maendeleo.

“Kongamano la Kwanza ka Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini limewakutanisha wadau takribani 1000 wakiwemo wanahabari, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kuwakutanisha wadau na kujadili maendeleo ya Sekta kwa ujumla aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, yaliyofanyika Mei 3, mwaka huu Jijini Arusha”, amesema Bw. Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.