Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

RAIS SAMIA APONGEZWA KWA KULETA SULUHU TANZANIA


Na Innocent Mungy, WHMTH, DAR ES SALAAM

Rais Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa kuleta suluhu nchini Tanzania kwa kuwaunganisha Watanzania bila kujadili itikadi zao, dini au jinsia katika kuiongoza Tanzania.

Hayo yalisemwa na mwanamuziki Judith Wambura Mbibo maarufu kama Lady Jay D wakati wa tamasha lake maalumu mwishoni mwa wiki la kumpongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuijenga Tanzania mpya inayojali uhuru wa watu, demokrasia na usawa pamoja na haki za binadamu.

“Mimi na mwenzangu Rama D tumeandaa wimbo huu na kuzindua kampeni ya “nasimama na Mama Samia” katika kuleta suluhu Tanzania ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo bila kujali itikadi zao, imani zao na kuhakikisha kuna uhuru wa kweli na demokrasia nchini” alisema Lady JD.

Akizungumza katika Tamasha hilo, Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Nnauye akliisema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anaongozwa na mambo manne makuu katika kusimamia maendeleo ya nchi na Watanzania kwa ujumla ambayo ni MARIDHIANO, USTAHIMILIVU, MAGEUZI, KUJENGA UPYA TANZANIA (Reconsiliation, Resiliency, Reforms na Rebuilding The Nation.)

Akizungumzia Maridhiano Mheshimiwa nape alisema Rais Samia anawaleta Watanzania pamoja bila kujali tofauti zao za kisiasa na kuhakikisha utawala wa sheria, usawa  na kutobaguliwa, na fursa sawa kwa wananchi wote kujiendeleza kibinafsi, jamii na taifa kwa ujumla zinafanyika. Pia alisema Mheshimiwa Rais katika utawala wake anahakikisha kuwa kila mtu anafurahia haki zake za msingi na kutekeleza majukumu yake kwa uhuru kwa mujibu  wa sheria bila kubughudhiwa na chochote na kwa uhuru.

Akizungumzia nguzo ya pili ya Ustahimilivu Mheshimiwa Nape alisema Rais Samia anaamini katika ustahimilivu kwa kuhakikisha raia wote wa tanzania wanapatanishwa na wanapaswa kupona kutokana na shida yoyote iliyokuwepo huko nyuma katika awamu zote za uongozi wa nchi yetu na kusonga mbele katika kuijenga Tanzania ya kesho. Aliongeza kuwa watanzania wote wanapaswa kukabiliana na changamoto za maendeleo kama taifa katika umoja na mshikamano na kuhakikisha nchi inasonga mbele kwa kujiamini.


Mageuzi ya msingi na muhimu ya kiuchumi, kisiasa na uchaguzi yatahakikisha sheria na haki nchini zinapatikana na ambazo kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakua na kuzalisha ajira kwa watu wake. Mageuzi haya yanapaswa kuimarisha juhudi zetu kuelekea kuwa na jamii yenye haki, kustawi kwa demokrasia na uchumi unaokua kwa faida ya Watanzania wote”, alisema Mhe. Nape alipozungumzia nguzo ya tatu ya mageuzi.

 Aidha Mheshimiwa Nape alizungumzia nguzo ya nne anayotumia Mama samia Suluhu hassan kuwa ni kuijenga upta Tanzania mpya. “Mama Samia, anahakikisha kuwa uchumi unakua ambao utazalisha ajira za kutosha kwa vijana wetu ni muhimu na ya kutosha ya kujenga upya Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania, kama hali ya ustawi wa karne ya 21 inayosisitiza kuwa maendeleo ni uhuru wa msingi. Ujenzi wa taifa ni mchakato unaohitaji uongozi unaoweza  kuimarisha suluhu baini ya wananchi wote”, alimalizia Mhe. nape Nnauye.

Tamasha hilo lilifanyika katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro na lilihudhuriwa na viongozi na wananchi mablimbali walioalikwa kuhudhuria. Katika Tamasha hilo, Lady JD pia alizindua Taasisi ya Binti itakayokuwa inahamasisha wanawake na hususani mabinti kusimama imara katika kuleta maendeleo yao bila kujali jinsia zao na kulalamika kuwa hawana nafasi katika shughuli za kujenga Tanzania.