Habari
POSTAMASTA MBODO ATOA WITO KWA NCHI ZA AFRIKA KUIMARISHA TEKNOLOJIA NA BIASHARA ZA MIPAKANI

Na Mwandishi Wetu – WMTH, Arusha
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Daniel Mbodo, ametoa wito kwa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU Administrative Council) kuhakikisha linaweka maazimio yenye malengo madhubuti ya kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuendeleza ubunifu wa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko huria. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukuza biashara za mipakani zitakazochochea ufanisi wa shughuli za mashirika ya posta katika nchi wanachama wa PAPU.
Bw. Mbodo alitoa kauli hiyo leo, Juni 18, 2025, jijini Arusha, alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, katika ufunguzi wa Kikao cha Kamati za Ufundi za Baraza la 43 la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU AC), kinachofanyika katika Jengo la Makao Makuu ya Umoja huo.
Akihutubia kikao hicho, Bw. Mbodo alisisitiza haja ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali kupitia mtandao wa posta, ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan walioko maeneo ya vijijini na pembezoni. Alieleza kuwa kwa kufanya hivyo, mashirika ya posta barani Afrika yatakuwa nyenzo muhimu ya maendeleo jumuishi na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika, Dkt. Sifundo Chief Moyo, alisema kuwa wananchi wa Afrika wana matarajio makubwa na imani kwa Umoja huo, hasa katika kuunganisha masoko yasiyo rasmi ya ndani na yale ya kimataifa. Alisisitiza kuwa ni muhimu huduma za posta ziwe za kisasa, zenye ufanisi, jumuishi na zinazowafikia watu wote bila ubaguzi.
Kikao hicho kimewakutanisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 22 wanachama wa PAPU, ambao watajadili mambo mbalimbali kupitia kamati hizo ikiwemo za Uendeshaji na Teknolojia , Fedha na Utawala, Sera na Kanuni na Mikakati.
Vikao hivi vya Kamati za Ufundi vinafanyika kuanzia leo Juni 18 hadi 20, 2025. Ambapo vitafuatiwa na Meza ya Duara kwa viongozi wakuu wa Posta (CEOs Round table) tarehe 23 Juni 2025, kabla ya kufikia kilele kwa Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Utawala la PAPU utakaofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 25 Juni 2025.