Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

POSTA, CHACHU YA MAENDELEO YA KIDIJITALI


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Mkapa, amesema kuwa Sekta ya Posta inaendelea kuwa chachu muhimu ya maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini kupitia matumizi ya teknolojia, ubunifu na ushirikishwaji wa wadau wote. 

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, alisema kaulimbiu ya mwaka huu “Posta kwa ajili ya watu: Huduma za Kizawa, Ufikaji Kimataifa” inaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za posta zinakuwa kiunganishi kati ya jamii na fursa za kijamii na kiuchumi.

Bw. Mkapa alisema Sekta ya Posta imepitia mageuzi makubwa kutoka kusafirisha barua hadi kuwa mhimili wa biashara mtandao na usafirishaji wa bidhaa, sambamba na jukumu jipya la kuwezesha uchumi wa kidijitali. 

Alilisifu Shirika la Posta Tanzania kwa kuweka mikakati ya kuboresha huduma, kutumia TEHAMA na kuongeza ubunifu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya dunia.

Katika maadhimisho hayo, washindi wa Shindano la Uandishi wa Barua Kimataifa na Shindano la Ubunifu wa Mifumo ya Huduma za Posta ambayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya watoto na vijana katika uandishi, ubunifu na mawasiliano walitangazwa na kutunukiwa zawadi. 

Kwa upande wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kuratibu mashindano ya ubunifu wa mifumo ya kusafirisha bidhaa, hatua inayowezesha vijana kutumia teknolojia kutatua changamoto za kisekta na kitaifa, kukuza ujasiri na uwezo wa kubadilisha mustakabali wa taifa kuelekea uchumi wa kidijitali.

Kuhusu Wiki ya Huduma kwa Wateja, Bw. Mkapa alisisitiza kuwa utoaji wa huduma bora si anasa bali ni wajibu wa kila taasisi kwa kuwa  huduma bora ni kipimo cha uadilifu na uwajibikaji wa taasisi kwa wananchi na kuwataka kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma.

Akihitimisha, alisema Wizara itaendelea kuwezesha Sekta ya Posta kupitia sera na kanuni bora, pamoja na kusimamia maendeleo ya TEHAMA ili kuhakikisha Tanzania ya kidijitali inakuwa halisi.