Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

PDPC KUANZA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA MUJIBU WA SHERIA


Na Georgina Misama, Maelezo

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ipo tayari kuanza kutekeleza majukumu ya tume hiyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Ndugu Abdulla amesema hayo leo Aprili 03, 2024 katika hafla ya uzinduzi  rasmi wa tume hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo alisema tume hadi sasa imeweza kukamilisha uundwaji wa mfumo wa usajili na upokeaji wa malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi.

“Serikali imeridhia utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya mwaka 2022, ambayo ilianza kutekelezwa Mei 01, 2023. Uwepo wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, una taswira ya kitaifa na kimataifa. Lengo la hafla hii ni kuujulisha umma kuwa Tume hiyo itaanza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusu ulinzi wa taarifa binafsi,” alisema Bw. Abdulla.

Alisema Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ina jukumu la kusimamia Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 na kwamba Sera hiyo imebainisha uwepo wa mifumo ya kisheria na  kitaasisi ambayo itaweka  mazingira wezeshi katika kuhakikisha TEHAMA inaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Adadi Rajabu alisema tayari tume imeanza kufanya mikakati maalum ya kuweza kujenga na kutoa elimu kwa umma kuhusu chombo hiki ambacho ni kigeni nchini Tanzania ili kuhakikisha kuwa Bodi uliyoteuliwa kusimamia Tume hiyo itahakikisha inafanya kazi zake kwa weledi mkubwa. Vilevile aliahidi kuhakikisha kuwa Tume hiyo  inalinda na inasimamia taarifa binafsi  kwa weledi mkubwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Bw. Emmanuel Mkilia, alisema; “Nakushukuru Mhe. Rais Samia kwa kutekeleza kwa vitendo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotaka haki ya faragha kwa kila Mtanzania, umewashika mkono Watanzania kwa kuwaletea sehemu ya kufikisha malalamiko yao yanayohusu uvunjifu wa faragha zao”.

Bw. Mkilia alisema kwamba hatua ya kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni kubwa na ya kihistoria na kwamba itafungua milango ya ushirikiano kati ya Tanzania na ulimwengu wa uchumi, kidiplomasia na kidijitali.