Habari
NINAHESHIMU MCHANGO WA VYOMBO VYA HABARI; WAZIRI SILAA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema anaheshimu mchango wa vyombo vya habari nchini, akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anathamini na kuendeleza sekta hiyo.
Waziri Silaa aliyasema hayo alipohutubia viongozi na washiriki wa Hafla ya Ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, uliofanyika leo, Novemba 18, 2024, katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Waziri Silaa alieleza kuwa Rais Samia ameendelea kutoa maelekezo muhimu kwa vyombo vya habari, na alipokuwa akimwapisha tarehe 26 Julai, 2024 alimuagiza kusimamia uhuru wa habari.
Alimpongeza Rais Samia kwa hatua alizochukua tangu awali, akirejea maelekezo aliyotoa tarehe 6 Aprili, 2021, ya kufungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa na kurejesha leseni kwa vyombo vilivyokamilisha adhabu zao.
Akizungumzia takwimu za vyombo vya habari nchini, Waziri Silaa alisisitiza kwamba Tanzania inavyo vyombo vingi vya habari, ikiwa ni pamoja na magazeti 179, majarida 174, vituo 247 vya redio, vyombo vya habari vya mtandao 355, na vituo 68 vya televisheni. Jumla ya vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini ni 1,023.
Waziri Silaa aliwakumbusha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, maadili, na misingi ya uandishi wa habari. Alisisitiza kuwa milango yake iko wazi na yuko tayari kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ili kuendeleza na kuimarisha vyombo vya habari nchini.
Mwisho, Waziri Silaa aliahidi kuendelea kukutana na taasisi na vyombo vya habari mmoja mmoja ili kujadili masuala mbalimbali na kuboresha sekta hiyo.