Habari
NIBA YATAKIWA KUWA KIUNGANISHI CHA SERIKALI NA VYOMBO VYA HABARI VYA BINAFSI

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma.
Serikali imekitaka Chama cha Watangazaji Huru Tanzania (NIBA) kuhakikisha kinakuwa chama chenye tija na kitakachosaidia kurahisisha mawasiliano baina yao na Serikali badala ya kuwa umoja wa kiharakati.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo tarehe 27 Septemba, 2024, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Mkapa, wakati wa hafla ya kufungua Mkutano Mkuu wa Pili wa NIBA, akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Jerry William Silaa (Mb).
Bw. Mkapa amewapongeza waanzilishi wa NIBA, akisema kuwa kuanzishwa kwa chombo hicho kutarahisisha mawasiliano kati ya Serikali na vyombo vya Habari hususan vyombo binafsi.
“Wekeni mbele maslahi mapana ya nchi, wekeni mbele uzalendo na kuipenda nchi yenu. Tusaidieni katika kuhakikisha amani na utulivu wa nchi unadumishwa,” amesema Naibu Katibu Mkuu Mkapa na kuongeza;
“Tunaamini uwepo wa chama hiki utaongeza tija na uwajibikaji wa vyombo vya utangazaji katika kufanikisha masuala muhimu ya nchi yetu,”
Amesisitiza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itaendelea kushirikiana na wadau muhimu katika sekta ya habari ili kupeleka taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu maendeleo yanayopatikana katika maeneo yao na mikakati mbalimbali ya serikali.
“Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria kwa lengo la kuwezesha sekta ya utangazaji kuwa imara na tegemeo la wananchi wa Kitanzania kupitia taaluma waliyoipata vyuoni,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu Mkapa amebainisha kuwa upo umuhimu mkubwa kwa NIBA kufanya kazi kwa karibu na TCRA, akielekeza kuwa ushirikiano huo uendelee.
“Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inakamilisha maboresho ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, ambayo inatarajiwa kujibu changamoto zote zilizotajwa katika risala yenu,” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu Mkapa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mhandisi Andrew Kisaka, Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji TCRA, Amosi Ngosha, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari vya Utangazaji Tanzania (NIBA), Habi Gunze, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini NIBA, Wamiliki na wawakilishi wa vyombo vya habari nchini.