Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE AHIMIZA KASI YA UJENZI WA JENGO LA WIZARA IONGEZEKE



 
Na Tagie Daisy Mwakawago, WHMTH
 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amefanya ziara ndogo katika jengo la Wizara hiyo na kutoa wito kwa wakandarasi wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) kuongeza kasi ya ujenzi, ili Watumishi waanze kuhamia katika ofisi hizo mapema iwezekanavyo.
 
Waziri Nape amesema hayo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi mpya za Wizara katika mji wa Serikali – Mtumba, tarehe 20 Januari 2023 jijini Dodoma. Viongozi wengine waliombatana na Waziri Nape kwenye ziara hiyo ni Wakurugenzi Watendaji wa Makampuni ya Simu Tanzania ya Vodacom, Airtel na Tigo.
 
Awali, Shirika la NHC lilitoa ahadi ya kukamilisha ujenzi huo mwezi Aprili 2023, miezi sita mapema kabla ya makubaliano ya mkataba wa ujenzi kuisha.
 
“Mradi huu una gharama za shilingi bilioni 23.9 kwa ujenzi wa muda wa miezi 24, ambapo ujenzi ulianza rasmi tarehe 22 Oktoba 2021 na unatarajiwa kukamilika tarehe 21 Oktoba 2023, amesema Meneja wa Mradi kutoka NHC, Mha. Grace Musita.  Wizara imeshalipa shilingi bilioni 7.9 katika ujenzi huo hadi kufikia sasa.
 
Mha. Musita, ameeleza kuwa kumekuwa na mfumuko wa bei za nondo, saruji na taratibu za manunuzi ambazo zimechangia ucheleweshwaji wa ujenzi kukamilika kama ilivyotarajiwa hapo awali.
 
Aidha, Waziri Nape ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake kwa kuhakikisha fedha zinatolewa katika kuwezesha ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali katika Mji wa Serikali yaliyopo Mtumba, jijini Dodoma.
 
Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Naibu Katibu wa WHMTH, Timu ya Menejimenti na Watumishi wa Wizara.