Habari
NAIBU WAZIRI MMUYA AHIMIZA MATUMIZI YA MFUMO WA NaPA KURAHISISHA HUDUMA NA UTOAJI WA TAARIFA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya (Mb), ametembelea banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kusisitiza umuhimu wa matumizi na huduma za kidijitali, hususan Mfumo wa NaPA, kuelekea michuano ya AFCON 2027.
Naibu Waziri Mmuya ameyasema hayo leo tarehe 18 Juni, 2026
alipotembelea Maonesho wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa uwepo wa mfumo imara wa Anwani za Makazi utarahisisha wageni, watalii na washiriki wa michuano hiyo kufika katika maeneo mbalimbali nchini kwa urahisi na usahihi, jambo litakaloboresha uzoefu wao wanapokuwa nchini.
“Mfumo wa NaPA ni nyenzo muhimu katika kuimarisha huduma za kidijitali na kurahisisha upatikanaji wa maeneo. Tunapaswa kuhakikisha wageni watakaokuja nchini kwa ajili ya AFCON 2027 wanapata urahisi wa kufika katika mtaa au eneo lolote bila changamoto,” amesema Mhe. Mmuya.
Aidha, Mhe. Mmuya ameishauri Wizara kuangalia uwezekano wa kuingia makubaliano na kampuni zinazoingiza simu nchini ili vifaa hivyo viweze kuunganishwa moja kwa moja na programu ya Mfumo wa NaPA tangu hatua za awali za matumizi. Amesema hatua hiyo itaongeza matumizi ya mfumo huo, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwezesha taasisi za umma pamoja na kampuni binafsi kutumia anwani sahihi za makazi katika shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wao, wataalamu wa Wizara wamemueleza Naibu Waziri Mmuya namna Mfumo wa NaPA unavyorahisisha utambuzi wa maeneo, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi, pamoja na kuchangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
