Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Naibu Waziri Mkama Akagua Mradi wa Mkongo wa Taifa Kuunganisha Tanzania na DRC.


Na Mwandishi wetu -WMTH

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Mkama (Mb.), amefanya ziara mkoani Kigoma tarehe 18 Agosti 2026, kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa unaolenga kuiunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika. Naibu Waziri alipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Mhe. Rashid M. Chuachua, kabla ya kuanza ziara yake katika Ofisi za TTCL Kigoma.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alitembelea maeneo mbalimbali ya ofisi za  TTCL na kukagua mitambo inayofanya kazi TTCL kwa Ukanda wa Kigoma. 

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi, Meneja wa Mradi wa Kuunganisha DRC, Mhandisi Emmanuel Temu, alisema kuwa mradi huo umegawanyika katika maeneo makuu matatu, ambapo asilimia 15 ya mradi inahusisha ujenzi upande wa Kigoma kwenye nchi kavu, asilimia 70 inahusisha sehemu ya majini kupitia Ziwa Tanganyika, huku asilimia 15 iliyobaki ikiwa upande wa DRC kwenye nchi kavu. 

Alieleza kuwa kwa sasa utekelezaji wa mradi upande wa Kigoma umefikia asilimia 5 kwa kutengeneza Beach Man Hall kwa ajili ya kuwezesha shughuli za kupokea na kusafirisha nyaya za Mkongo wa Taifa kuelekea DRC kupitia Ziwa Tanganyika, wakati upande wa DRC tayari wamefanya tathmini na kupata vibali vinavyohitajika kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Mhandisi Temu aliongeza kuwa Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo, huku akieleza kuwa Mkongo wa Taifa unaounganisha Tanzania na DRC unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2027.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri Dkt. Mkama alisisitiza umuhimu wa mradi huo kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, akieleza kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya mawasiliano. Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha mawasiliano ya kidijitali kati ya Tanzania na DRC, kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti na kufungua fursa zaidi za kiuchumi na kijamii kupitia teknolojia.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha miradi ya kimkakati ya mawasiliano inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati. Mkongo huo unatarajiwa kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya Tanzania na DRC, huku sehemu kubwa ya mradi ikipita majini kupitia Ziwa Tanganyika, na hivyo kuimarisha nafasi ya Tanzania katika kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati kupitia miundombinu ya kisasa ya TEHAMA.