Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU WAZIRI MHANDISI KUNDO AZURU NGARA KUKAGUA MWINGILIANO WA MAWASILIANO MIPAKANI


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kulia) akizungumza katika eneo la mpaka wa Kabanga Wilayani Ngara eneo ambalo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umefika na kuunganisha nchi ya Burundi wakati wa ziara yake ya kukagua changamoto za mwingiliano wa mawasiliano katika mpaka huo. Wa pili kulia ni Mbunge wa Ngara Mhe. Ndaisaba Luhoro

 

NGARA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amefanya ziara katika wilaya ya Ngara iliyopo Mkoa wa Kagera kwa lengo la kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika wilaya hiyo ambayo inapakana na nchi jirani ya Burundi kwa upande wa mpaka wa Kabanga na Rwanda katika mpaka wa Rusumo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua changamoto za mawasiliano katika maeneo ya mipaka yenye mwingiliano wa mawasiliano na nchi jirani

Akiwa ziarani katika wilaya hiyo tarehe 02/08/2021 amesema kuwa Wizara hiyo kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetangaza zabuni ya jumla ya shilingi Bilioni 1.3 ya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika kata tisa za wilaya hiyo ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika wilaya hiyo. Kata hizo ni Bugarama, Butililo, Kabanga, Kasulo, Kibogola, Mabawe, Mutulazo, Nyakisasa na  Nyamagoma

Amesema kuwa Wilaya hiyo ni moja ya maeneo ya mipakani ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wabunge kuhusu changamoto za mwingiliano wa mawasiliano na nchi jirani ndio sababu ya yeye kufika katika wilaya hiyo akiambatana na wataalam wa Wizara hiyo  pamoja na taasisi zake kwa lengo la kuangalia uhalisia wa changamoto hizo

Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuimarisha huduma ya mawasiliano katika mipaka ya Tanzania kwasababu mipaka hiyo inabeba taswira ya uchumi wa nchi na pia masuala ya usalama na kuwapatia fursa watanzania kuona kile ambacho kinatokea ndani ya nchi yao kw akua unapoongelea mawasiliano inajumuisha mawasiliano ya redio na runinga

Aidha, amesema kuwa wananchi waishio katika maeneo ya mipakani wamekuwa wakitumia gharama kubwa kupata huduma za mawasiliano kupitia huduma ya roaming kutokana na mwingiliano wa mawasiliano na kupelekea kuchangia mapato ya nchi jirani kupitia huduma hiyo

Naye Mbunge wa Ngara Mhe. Ndaisaba Luhoro ameishukuru Serikali kwa kuidhinisha matumizi ya shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kujenga minara ya mawasiliano katika Wilaya hiyo ambayo imekuwa na changamoto kubwa ya mwingiliano wa mawasiliano na mitandao ya nchi jirani za Rwanda na Burundi

Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo alitembelea ofisi za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wilayani Ngara na kukuta jengo la ofisi za Shirika hilo likiwa na wapangaji ambao ni chuo, kanisa na taasisi ya umma ya TRA huku Shirika la TTCL likiwa linatumia chumba kimojawapo nyuma ya jengo hilo bila kuwepo kwa alama yeyote inayoonesha uwepo wa Ofisi ya TTCL katika jengo hilo

Aidha, Mhandisi Kundo alikutana na malalamiko ya huduma ya choo kutoka kwa wapangaji wa jengo hilo kuwa vyoo vilivyopo havitoshelezi mahitaji kwasababu jengo hilo lina vyoo viwili tu wakati idadi ya watu wanaotumia huduma hiyo ni wengi ikijumuisha wanafunzi wa chuo. Hata hivyo, ilifahamika kuwa malalamiko hayo yaliwasilishwa katika ofisi ya TTCL Mkoa wa Kagera ambapo waliahidi kutatua kero hiyo lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika

Sambamba na hilo Mhandisi Kundo ametoa rai kwa mameneja wa mikoa wa TTCL kutoka ofisini na kutembelea matawi ya Shirika hilo katika ngazi ya wilaya ili kufatilia kwa karibu hali ya biashara za shirika pamoja na kutatua kero zinazojitokeza. Mhandisi Kundo ametoa rai hiyo baada ya kupata taarifa na kuthibitisha kuwa Meneja wa Mkoa huo hakuwahi kufika katika Ofisi za Shirika zilizopo katika wilaya ya Ngara toka mwaka 2021 uanze