Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU WAZIRI KUNDO ARIDHISHWA NA UJENZI WA OFISI YA WIZARA


Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na watumishi wa Wizara hiyo wakati alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za Wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, leo tarehe 26 Agosti, 2022 

DODOMA

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ameridhishwa na  maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wizara hiyo unaoendelea kufanyika alipotembelea na kukagua ujenzi huo Agosti 26, 2022 katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Mhandisi Kundo amepongeza timu nzima ya wataalamu wa kandarasi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kufanya kazi kwa weledi, kujitoa pamoja na ubunifu utakaorahisisha  ujenzi kumalizika mapema kabla ya muda wa mkataba.

“Mradi  huu  wa ujenzi wa ofisi ya Wizara umefikia asilimia 43 ikiwa ni miezi 10 tangu mradi huu uanze kutekelezwa na unatarajiwa kumalizika ndani ya miezi sita kuanzia sasa  kama mkandarasi alivyoahidi”, amesema Mhandisi Kundo

 Ameongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo umezalisha ajira za muda mfupi zaidi ya 160 kwa watanzania ikiwa ni moja ya manufaa ya ujenzi wa ofisi mbalimbali za Serikali zinazoendelea kujengwa katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

“ Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kufanikisha ujenzi wa ofisi za serikali ambao pamoja na mambo mengine zimezalisha ajira za muda mfupi kwa wananchi na kuwaingizia kipato kwa ajili ya mahitaji yao na familia zao”, amezungumza Naibu Waziri huyo.

Aidha, Mhandisi Kundo amewataka kuwa makini katika ukamilishaji kazi hiyo na kuwakumbusha asilimia zilizobaki ni nyingi na kuwaomba wazingatie muda na ubora  katika kukamilisha jengo hilo.

Naye Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi wa Wizara hiyo Armon MacAchayo amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuongeza kasi zaidi bila kuathiri ubora na viwango vya ujenzi wa jengo hilo ili kumaliza ujenzi kabla ya muda wa mkataba.

Ujenzi wa jengo la  ofisi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari unatarajiwa kugharimu zaidi ya billion 23 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi billion 8 sawa na asilimia 23 ya malipo ya jengo nzima zimekwishatumika.

Amesema kuwa katika ujenzi wa jengo hilo kumezalishwa ajira zaidi ya 160  kwa watanzania ambao wanafanya kazi eneo hilo na kumshukuru  Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika uzalishaji wa ajira kwa familia za watanzania wanaofanya kazi katika mji huo wa mtumba na kuwataka watanzania wawe wazalendo.