Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU WAZIRI ATAKA MKANDARASI KUFUATA VIGEZO VYA UJENZI WA MKONGO WA MAWASILIANO


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ametoa maelekezo kwa Mkandarasi wa kampuni ya Raddy Fibre anayejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 72 kutoka Mangaka hadi Mtambaswala kuzingatia vigezo vilivyowekwa vya ujenzi wa muundombinu huo ili usiharibu wala kuharibiwa na miundombinu ya barabara za TARURA, TANROAD pamoja na miundombinu ya maji

 

Maelekezo hayo ameyatoa alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mkongo huo unaoendelea katika wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara kwa lengo la kuimarisha huduma za mawasiliano mpakani hasa kuunganisha mawasiliano baina ya nchi ya Tanzania na Msumbiji

 

“Mkandarasi yeyote anayepewa zabuni ya kujenga na kuendeleza miundombinu ya Serikali anatakiwa kufanya kazi kwa kufuata masharti ya mkataba na kutoa taarifa sahihi za mradi anaotekeleza ili Serikali iendelee kuwaamini Makandarasi wazalendo kuwa wanakidhi vigezo vya kutekeleza miradi ya maendeleo na kujenga nchi yetu sisi wenyewe”, alizungumza Mhandisi Kundo

 

Ameongeza kuwa ameona baadhi ya mapungufu katika ujenzi wa Mkongo huo hasa kwa upande wa kina kinachotakiwa kuchimbwa kwa ajili ya kuweka muundombinu huo na kumuelekeza mkandasari kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi na atakwenda kukagua tena ili kujiridhisha

 

Naye Mbunge wa Nanyumbu Mhe. Yahya Mhata amesema kuwa ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaoendelea kufanyika kuanzia Mangaka mpaka Mtambaswala umetengeneza ajira za muda mfupi kwa vijana wa jimbo lake na kuwasaidia kujiingizia kipato ikiwa ni alama kuwa Serikali inawajali wananchi wake

 

Kwa upande wa Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Raddy Fibre Mohamed Mlanzi amesema kuwa amepokea maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri na kuahidi kufanya maboresho maeneo yote ambayo yanahitaji maboresho

 

Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika eneo la Mangaka hadi Mtambaswala una gharama ya shilingi Bilioni 2.4 ambapo kilomita 68 kati ya kilomita 72 zimeshakamilika na kituo kimoja cha kusambaza huduma ya Mkongo kimeshajengwa kwa asilimia 94.