Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU WAZIRI AKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA KWA AJILI YA SHULE ZA SEKONDARI ZA MKOA WA SHINYANGA


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kulia) akikabidhi kompyuta kwa Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Shinyinga Mhe. Mhe. Santiel Kirumba (wa kwanza kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Janista Mboneko na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Shinyanga Nice Munisi

 

SHINYANGA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya shule 6 za Sekondari zilizopo ndani ya Mkoa wa Shinyanga vyenye thamani ya shilingi Milioni 50 vilivyotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)

Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe 14.08.2021 Mkoani Shinyanga kati ya Naibu Waziri huyo na Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Santiel Kirumba, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Janista Mboneko, na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Shinyanga Nice Munisi ambapo jumla ya kompyuta 30 na printa 4 zilikabidhiwa rasmi

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo Mhandisi Kundo amesema kuwa Serikali kupitia UCSAF imeendelea kutekeleza mradi wa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma ili kuchochea ukuaji wa matumizi ya TEHAMA na kuwaandaa vijana na mabadiliko ya teknolojia duniani

Sambamba na hilo amezungumzia mradi wa wasichana na TEHAMA unaotekelezwa na UCSAF ambao unalenga kuwawezesha na kuwajengea uwezo watoto wa kike katika TEHAMA ndio maana katika upelekaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule za sekondari Mfuko huo unaangazia  na Shule za Sekondari za wasichana

“Wizara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tuna kipengele kingine cha kuwawezesha watoto wa kike na TEHAMA ili kuwajengea uwezo na hatimaye kutengeneza wataalam wa TEHAMA wengi zaidi nchini kwa sababu mpaka sasa wataalam wa TEHAMA wanawake ni wachache kuliko wa kiume lengo letu ni kwamba tunapoongelea 50 kwa 50 ionekane kwa vitendo”, amesema Mhandisi Kundo

Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo huyo ameushukuru uongozi mzima wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Wizara hiyo huku akimtaja Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Philemon Sengati na wasaidizi wake ambao wamekuwa ni chachu ya mtazamo chanya katika kukuza matumizi ya TEHAMA nchini

Aidha, Naibu Waziri huyo ametoa rai kwa viongozi na wasimamizi wa vifaa hivyo kuhakikisha vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Wizara kupitia taasisi yake ya UCSAF itakuwa inapita kuangalia kama zinatumika na kuleta matokeo tarajiwa kwa walimu na wanafunzi wa shule hizo

Naye Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Kirumba amesema kuwa kompyuta hizo zitaenda kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi na kuongeza ufaulu wa shule hizo ameishukuru na kuipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara hiyo na taasisi yake ya UCSAF kwa kuthamini na kuisimamia vema ilani ya uchaguzi ambayo imezungumzia kuongeza matumizi ya TEHAMA na wao wanatekeleza kwa vitendo

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Mboneko ameishukuru Wizara na UCSAF kwa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika wilaya yake na kumhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa vifaa hivyo watavilinda na kuhakikisha vinaendelea kutumika ipasavyo pamoja na kutoa taarifa ya maendeleo ya TEHAMA katika Wilaya hiyo

Kwa Upande wa Mkuu wa Uendeshaji wa UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema kuwa vifaa hivyo vya TEHAMA vilivyokabidhiwa katika Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa jumla ya kompyuta 800 na printa 20 zinazoendelea kusambazwa katika ya shule za sekondari za umma ambazo zilianishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/22