Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU KATIBU  MKUU WA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI ATEMBELEA SHIRIKA LA POSTA


 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdullah amelipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma zake pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anapata Huduma stahiki na zenye ubora.

Bw. Abdullah alisema hayo wakati wa ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya Shirika hilo tarehe 18 Julai 2022 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya mazungumzo na Meneja wa Posta Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Arubee Ngaruka,  Postamasta Mkuu wa Shirika hilo Bw. Macrice Mbodo na wafanyakazi wengine wa Shirika hilo.  Naibu Katibu Mkuu alipata taarifa mbalimbali za uendeshaji wa Shirika la Posta na huduma zinazotolewa katika maeneo ya usafirishaji wa barua, nyaraka, mizigo na vipeto.

Naibu Katibu Mkuu pia alitembelea kituo cha "Huduma Pamoja" kinachotoa huduma za Serikali kwa wananchi mahali pamoja zikiwemo zile zinazotolewa na NIDA, TRA, RITA, NHIF na Uhamiaji, kilichopo katika ofisi za Shirika la Posta Tanzania, jijini Dar es Salaam. 

Shirika la Posta Tanzania lilianzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kutoa huduma za posta ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuiunganisha Tanzania na Dunia kwa dhamira ya kutoa Huduma Bora za posta kwa wote zitakazokidhi matarajio ya wateja.