Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MSISUBIRI KWENDA KUJITETEA - WAZIRI NAPE


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dae es Salaam.

Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhe.Nape Nnauye (Mb) amewataka maafisa Habari,Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati na kuacha utamaduni wa kusubiri mpaka taarifa za upotoshaji zitokee ndio watoe taarifa za kujitetea.

Waziri Nape ameyabainisha hayo Leo Machi 29, 2023 wakati akizungumza katika kikao kazi cha 18 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kinachoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Tuulishe umma taarifa sahihi na kwa wakati, ukiona inafikia hatua unatakiwa kutoa taarifa ya kujitetea basi ujue kuna mahali unakosea”, Amezungumza Waziri Nape.

Ameongeza kuwa, “Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano ndio mmebeba taswira na mitazamo ya taasisi zenu, taswira na mitazamo inatengenezwa hivyo ni wajibu wenu kutengeneza mitazamo chanya ya taasisi mnazotumika”.

Amesisitiza kuwa, kada ya maafisa habari ina umuhimu wa kipekee na iwapo wakitimiza majukumu yao ipasavyo wataongeza thamani na umuhimu wao katika taasisi wanazofanya kazi.

“Nimepokea changamoto zenu za bajeti na vitendea kazi, sasa nitoe wito kwenu wa kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu ili ninapoenda kupigania haki zenu na nyie muwe mmeonesha thamani ya uwepo wenu”, amezungumza Nape.

“Uafisa habari ni ajira, ni jukumu la kulinda taswira ya taasisi yako, na pia ni fursa ya kubadili maisha binafsi na Taifa kwa ujumla iwapo ukifanya vizuri katika eneo lako”, amezungumza Waziri huyo.