Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI WAFIKIA 90% YA UTEKELEZAJI


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Mohamed Mashaka, amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali umeiwezesha nchi kujiweka katika ramani ya ushindani wa kimataifa katika nyanja za teknolojia ya kidijitali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari wakati wa kikao cha  tathmini ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Mashaka alisema kuwa mradi huo umejikita katika kuwezesha Serikali kutoa huduma za kidijitali kwa wananchi kwa haraka, uwazi na ufanisi zaidi.

“Lengo kuu la TEHAMA ni kurahisisha maisha ya wananchi, na huo ndio msingi wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali,” alisema Bw. Mashaka.

Alibainisha kuwa sekta ya mawasiliano ni nguzo muhimu ya maendeleo, kwani huifanya dunia kuwa kijiji kupitia uchumi wa kidijitali, na hivyo kuchangia katika ustawi wa kijamii na kiuchumi wa taifa pamoja na wananchi mmoja mmoja. Aidha, alisisitiza kuwa hakuna Mtanzania au taasisi ya umma itakayosalia nyuma katika mapinduzi haya ya kidijitali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Bw. Priscus Kiwango, alisema kuwa kupitia mradi huu, watumishi wa umma katika taasisi mbalimbali wanapatiwa mafunzo ya kutumia mifumo ya kidijitali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Bakari Mwamgugu, alieleza kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia takriban asilimia 90, huku hatua muhimu zikiwa zimekamilika.

“Tumefanikisha hatua mbalimbali, zikiwemo upanuzi wa miundombinu ya TEHAMA, utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa umma, na kuunganisha taasisi za umma kwenye mifumo ya kidijitali,” alisema Bw. Mwamgugu.

Aliongeza, minara 758 ya mawasiliano inayoendelea kujengwa nchini kote kupitia mradi huo, inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za Serikali kwa njia ya kidijitali, hata akiwa maeneo ya vijijini.

Mradi huu wa miaka mitano unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia, na unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 150. Utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026.