Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MRADI WA MINARA 758 WAIPA TANZANIA TUZO YA KIMATAIFA YA WSIS 2026


Tanzania imepata heshima ya kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya WSIS Prizes 2026 kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ulioongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na ambayo hayakuwa na huduma ya mawasiliano nchini.

Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki(Mb.) katika hafla iliyofanyika Geneva, Uswisi, tarehe 10 Julai, 2026 ikiwa ni utambuzi wa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Miundombinu ya Mawasiliano.

 

Mbali na kutwaa tuzo hiyo, Tanzania ilipata uteuzi katika vipengele saba (7) vya Tuzo za WSIS 2026 na kufanikiwa kuibuka na tuzo mbili kwa ujumla, huku pia ikitunukiwa vyeti vya kutambua miradi iliyofanya vizuri.

 

Ikumbukwe kuwa, Mradi wa Minara 758 ulizinduliwa rasmi na Mhe. Rais tarehe 10 Aprili, 2026 jijini Dodoma na leo unatambuliwa kama moja Miradi kinara unaowezesha nchi ya Tanzania kuendeleza matumizi ya Teknolojia ya Kidijitali kwa haraka na kasi zaidi.