Habari
MRADI WA DTP KUMALIZA CHANGAMOTO ZA MAWASILIANO ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar - Dkt. Mzee Suleiman Mndewa amesema ifikapo 2026 Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigitali inaenda kumaliza changamoto zote za mawasiliano Visiwani Zanzibar.
Dkt. Mndewa amesema hayo leo tarehe 26 Agosti, 2024 jijini Arusha wakati wa kikao cha kufanya tathmini ya Mradi wa Tanzania ya Kidigitali (DTP) kwa nusu muhula.
Amesema ifikapo 2026 sekta ya Mawasiliano Zanzibar haitokuwa na changamoto yoyote kwakua kupitia mradi wa DTP wanaenda kuwagusa wananchi wapate huduma zote za kiserikali kupitia TEHAMA, hivyo Serikali itaboresha sehemu zote ambazo Miundombinu ya Mawasiliano sio rafiki.
"Tunaenda kujenga Minara, kwa mfano katika maeneo ya vijijini, usikivu au upatikanaji wa Intaneti unaenda kuboreshwa ili wananchi waweze kupata huduma kwa kiwango cha juu. Kwa hiyo ifikapo 2026, sehemu zile ambazo zimekusudiwa kuwekewa Mawasiliano zitawekewa" amesema Dkt. Mndewa.
Kwa upande wake Bw. Paul Seaden, Kiongozi wa Kikosi kazi kutoka Benki ya Dunia amesema amefurahishwa na maendeleo ya Mradi wa DTP unavyofanyika kwa kuwa umeleta matokeo chanya kwenye sekta ya TEHAMA nchini.
"Kumekua na maendeleo mazuri na mafanikio mengi kwenye maeneo muhimu kama vile maeneo ya Miundombinu na kwenye Taasisi za TEHAMA, kwa hivyo tunaangalia namna mradi huu utakavyokamilika ifikapo Novemba, 2026", amesema Bw. Seaden