Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Itaendelea Kufuatilia Mwenendo wa Soko ili Kuhakikisha Huduma za Mawasiliano Zinakuwa Nafuu


Na Mwandishi Wetu, WMTH  Dodoma

Serikali imesema itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la mawasiliano na kuchukua hatua stahiki za kisera na kikanuni ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu, huku sekta hiyo ikiendelea kuchangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 27, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb) wakati akijibu swali la Mbunge wa Momba, Mhe. Condester Michael Sichwale, aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kupunguza gharama za vifurushi kwa kampuni zote za simu.

Mhe. Dkt. Mkama alisema Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu kwa wananchi, na kwamba Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zake, ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuboresha sekta hiyo.

Alizitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kusimamia ushindani wa haki miongoni mwa kampuni za simu ili kuchochea ubunifu na upatikanaji wa vifurushi vya gharama nafuu, kufanya mapitio ya gharama na tozo mbalimbali ili kulinda mlaji wa mwisho, pamoja na kuhimiza matumizi ya miundombinu ya pamoja ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Mhe. Dkt. Mkama aliongeza kuwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara, pamoja na vituo vya kuhifadhi data.

Kwa mujibu wa Dkt. Mkama, hatua hizo zimechangia kupungua kwa gharama za huduma za mawasiliano, hususan huduma ya intaneti ya faiba majumbani na maofisini.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma bora kwa gharama nafuu na sekta hiyo inakuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.