Habari
MKUU ABDULLA AZINDUA MAFUNZO YA JUU YA AKILI UNDE UDOM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, leo tarehe 15 Septemba 2025, amezindua rasmi mafunzo ya muda mfupi ya Kozi ya Juu ya Masuala ya Akili Unde (Advanced Artificial Intelligence Training) ikiwa ni mafunzo ya tatu kufanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mafunzo hayo yanayotarajiwa kudumu kwa siku 14, yamewaleta pamoja wataalam 20 wa TEHAMA kutoka sekta mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bw. Abdulla aliwapongeza washiriki kwa kupata nafasi hiyo adimu na kuwataka kutumia ujuzi watakaoupata kuleta manufaa ya moja kwa moja katika jamii ya Kitanzania.
“Wizara inatamani kuona matokeo chanya ya mafunzo haya, ikiwemo kuimarika kwa matumizi ya akili unde katika sekta za kijamii na kiuchumi nchini,” alisema Abdulla.
Aidha, Katibu Mkuu alikisihi Chuo Kikuu cha Dodoma na washirika wake kupitia Maabara ya Akili Unde kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya washiriki katika mafunzo yajayo, akieleza kuwa waliopo sasa ni wachache ikilinganishwa na mahitaji ya Taifa.
Katika hotuba yake, Bw. Abdulla pia alipongeza mwitikio mkubwa wa wanawake kushiriki katika kozi hiyo, akisema hatua hiyo ni kielelezo cha uongozi wa wanawake katika mapinduzi ya TEHAMA na ubunifu.
Akielezea jitihada za Serikali za kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya akili unde nchini, Katibu Mkuu huyo amesema Wizara hiyo ipo katika hatua za mwisho za uandaaji Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Akili Unde.
Huku akiainisha jitihada nyingine kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Maabara ya Akili Unde UDOM tangu mwaka 2021 pamoja na Ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (DTI) ambacho kitaleta mapinduzi katika kukuza wataalam na wabunifu wa TEHAMA.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, jitihada hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa zinazotolewa na teknolojia ya akili Unde katika kukuza uchumi wa kidijitali.