Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO NI MUUNDOMBINU MUHIMU WA TEHAMA UTAKAOSAIDIA NCHI KUUFIKIA UCHUMI WA KIDIJITI- DKT. YONAZI


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi ameuzungumzia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwa ni muundombinu muhimu wa TEHAMA utakaosaidia kuifikisha nchi katika uchumi wa kidijiti ambao ni uchumi shindani utakaoleta tija kwa nchi na mwananchi moja moja.

Dkt. Yonazi ameyazungumza hayo januari 27, 2023 jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya kutunza na kuendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kuwakabidhi vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo washiriki 114 kutoka TTCL na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Ameongeza kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye ujenzi na usambazaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na kuongeza uwezo na ustahimilivu wake katika utoaji wa huduma ambapo kiasi cha shilingi bilioni 170 za kitanzania zinatekeleza ujenzi wa muundombinu ya Mkongo wa Taifa kwa mwaka wa fedha unaoendelea kutekelezwa.

Aidha amewataka wataalamu hao waliopatiwa mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia taaluma zao kutekeleza majukumu yao ya kusimamia na kuendesha miundombinu ya Mkongo pamoja na kushauri ili Mkongo wa Taifa uendelee kuwa bora unaoleta ushindani katika uchumi na kutoa huduma bora ndani na nje ya nchi.

Naye Mtaalamu mshauri wa Ujenzi wa Mkongo, Bw. Emmanuel Nagunwa amesema mafunzo hayo ni muhimu na yanatakiwa kutolewa mara kwa mara kwa kuwa teknolojia inabadilika na watu wanabadilika hivyo ni muhimu kupanua wigo wa wataalamu wenye uwezo wa kusimamia, kutunza na kuendesha mitambo ya Mkongo wa Taifa ili iweze kutoa huduma bora na kuleta manufaa kwa Taifa.

Mkurugenzi Msaidizi wa HUAWEI Tanzania, Bw. Tom Tao  ameuzungumzia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwa ndio msingi wa uchumi wa kidijiti kwasababu ili kuweza kutumia teknolojia ya 5G, mifumo ya TEHAMA pamoja na matumizi ya teknolojia nyingine zinazovumbuliwa inategemea uwepo wa intaneti ya kasi kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Baadhi ya wataalamu walioshiriki mafunzo hayo wameyazungumzia mafunzo kusaidia na kuzidi kuwaimarisha katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia mahitaji na teknolojia ya vifaa na mitambo ya kuendesha na kutoa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.