Habari
MKOA WA MBEYA WAANZA UHAKIKI WA ANWANI ZA MAKAZI, WANANCHI WATAKIWA KUTUMIA MFUMO WA NAPA KIDIJITALI

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomoni Itunda, amewataka viongozi na wananchi kushirikiana kuhakikisha mfumo wa kidijitali wa Anwani za Makazi (NaPA) unafanya kazi kwa ufanisi na endelevu.
Akizungumza leo wakati wa akizindua rasmi zoezi la uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mhe. Itunda amesema zoezi hilo litatanguliwa na mafunzo maalum kwa viongozi wa mitaa ili kuwajengea uwezo wa kusimamia na kutekeleza zoezi husika.
Amesisitiza kuwa mafunzo watakayopatiwa yatumike kuwasaidia wananchi kuelewa na kutumia mfumo huo kama ilivyokusudiwa na kuchochea maendeleo.
Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa matumizi ya mfumo wa Anwani za Makazi ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya 2050 na ajenda ya kimataifa ya 2030 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Bi. Josephine Mwaijande, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amesema mfumo wa NaPA na mifumo mingine ya kisekta inayotoa huduma za kijamii.
Amebainisha kuwa, hadi tarehe 21 Septemba 2025, jumla ya barua 668,000 za utambulisho zimetolewa kidijitali nchi nzima kupitia mfumo wa NaPA, huku kwa Jiji la Mbeya pekee likiwa na maombi 14,325, ambayo yameshughulikiwa kikamilifu.
“Dhamira ya Serikali ni kila mwananchi ajue na atumie anwani yake ya makazi katika kupokea huduma, ikiwa ni hatua muhimu ya kuboresha utoaji wa huduma na mipango ya maendeleo,” amesema Bi. Mwaijande.
Amesisitiza kuwa, mfumo wa NaPA ni daftari rasmi la kidijitali kwa mitaa na vijiji, na kila mtendaji ana jukumu la kuhakikisha kila mkazi katika eneo lake amesajiliwa na taarifa zake ziko sahihi.