Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO KUCHOCHEA UCHUMI WA KIDIJITALI: SERIKALI YAONGEZA KASI YA DIRA YA 2050


Na Mwandishi wetu, WMTH - Dodoma.

 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano ili kuchochea uchumi wa kidijitali na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,  ikilenga kuifanya sekta ya mawasiliano kuwa nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumza wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Minara 758 ya Mawasiliano na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema uwekezaji huo utasaidia kupunguza pengo la kidijitali mijini na vijijini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano kwa usawa.

 

Ameeleza kuwa miundombinu hiyo ni kichocheo cha ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo biashara, elimu, afya na huduma za kifedha, kwa kuwezesha matumizi ya teknolojia za kidijitali. Hivyo, wananchi watanufaika kwa kuongeza kipato na kuboresha huduma za kijamii.

Rais Samia ameongeza kuwa Serikali pia imeweka mazingira rafiki kwa uwekezaji wa sekta binafsi na kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti, huku ikilenga kuongeza ufanisi wa Serikali mtandao na kuimarisha mawasiliano ya taasisi za umma kupitia upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

 

“Miundombinu hii ni msingi wa mageuzi ya kiuchumi. Tunataka kuona Watanzania wanatumia teknolojia hii kuongeza kipato, kuboresha huduma za kijamii na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa,” alisisitiza Mheshimiwa Rais.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb) amewapongeza Watoa Huduma za Mawasiliano na wadau wote muhimu wa Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa namna walivyoshiriki katika utekelezaji wa Miradi hii muhimu kwa Maendeleo ya Taifa.

 

Vilevile, ameongeza kuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kusimamia Mikakati mbalimbali ya kisekta ikiwemo Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Mwaka 2024 – 2034 na Mkakati wa Taifa wa Mtandao wa Kasi (Broadband Strategy 2021 - 2026) ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua katika masuala ya TEHAMA na ukuaji wake.

 

Kwa ujumla, uwekezaji huu unaifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano kikanda, huku ukichochea ubunifu na fursa kwa vijana na wajasiriamali. Wananchi wamehimizwa kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na maendeleo hayo ili kukuza uchumi jumuishi.