Habari
MIUNDOMBINU BORA YA MAWASILIANO KUWEZESHA UCHUMI WA DIJITALI

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akizungumza na wananchi wakati wa Ziara yake ya kukagua miundombinu ya mawasiliano katika Wilaya ya Serengeti
SERENGETI
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amezungumzia miundombinu ya mawasiliano kama barabara ambayo itaifikisha nchi katika uchumi wa dijitali kwa sababu ndio inayowezesha mawasiliano ya simu na intaneti hivyo ziara yake imejikita katika kukagua ujenzi, ubora na uwezo wa miundombinu ya mawasiliano na upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti katika maeneo mbalimbali nchini
Amesema kuwa kuongezeka kwa mtandao wa miundombinu ya mawasiliano nchini yenye ubora na uwezo wa kutoa huduma bora za mawasiliano kutawezesha wananchi wengi zaidi kushiriki katika shughuli za uchumi na biashara kwa njia ya mtandao; Sekta ya Umma na Binafsi kutoa huduma zake kwa njia ya mtandao na hatimaye kukuza uchumi wa dijitali
Mhandisi Kundo amezungumza hayo akiwa katika ziara ya kikazi Wilaya ya Serengeti ambapo ameainisha maeneo ambayo anakagua ni pamoja na kujiridhisha kama kusudi la miradi limetekelezwa kwa mfano kama mradi ulilenga kutoa huduma ya mawasiliano katika vijiji vitano yeye pamoja na ujumbe wake wanajiridhisha kama huduma ya mawasiliano inafika katika vijiji hivyo
Sambamba na hilo amezungumzia huduma ya intaneti kuwa ni huduma ya msingi kwa kila mwananchi hivyo katika ziara yake wanaangalia uhitaji wa huduma ya intaneti katika maeneo ambayo yana mawasiliano ya simu pekee yaani minara yenye teknolojia ya 2G na kujiridhisha uhitaji wa kubadilisha teknolojia iliyopo kwenda 3G na kuendelea ili kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya intaneti
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatoa ruzuku kwa makampuni ya simu ili kuweka unafuu na kupunguza gharama za uwekezaji wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini, mipakani na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa biashara ikiwa ni mkakati endelevu wa kuhakikisha watanzania wote wanafikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu na intaneti
Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo amesisitiza makampuni ya simu kufuata viwango vya ujenzi wa minara ya mawasiliano kwa kuhakikisha kunakuwa na choo, kibanda cha mlinzi na mlinzi ili kuimarisha usalama wa vifaa kwasababu ikitokea vikaibiwa itarudisha nyuma jitihada zinazofanyika na kupata hasara ya kurudia kufanya uwekezaji ambao ungeweza kufanyika katika maeneo mengine
“Tunafuatilia na kujiridhisha nani anatoa taarifa sahihi na nani hatoi taarifa sahihi lengo letu ni kuondoa kabisa changamoto na kero ambazo wananchi wamekuwa wakizilalamikia katika miradi yetu ya mawasiliano na katika maeneo ambayo Wizara imepewa dhamana ya kusimamia” alimalizia Mhandisi Kundo akizungumzia changamoto na kero anazokutana nazo kutoka kwa wananchi na kuzitafutia ufumbuzi