Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MIRADI YA MAENDELEO YA TEHAMA IGUSE MAISHA YA WATANZANIA


Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mha. Mathew Kundo akizungumza wakati akifunga mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika jijini Dodoma.

DODOMA

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo kuielewa miradi ya kitaifa inayotekelezwa na Wizara hiyo na kutafsiri ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo yanakuwa na manufaa; yanagusa maisha ya watanzania na inaleta fursa za kijamii, kiuchumi na kiteknolojia kwa wananchi

Naibu Waziri huyo ameyazungumza hayo leo tarehe 26 Machi, 2022 akifunga baraza la wafanyakazi la Wizara hiyo jijini Dodoma kwa kusisitiza watumishi wa Wizara hiyo kuelimishana kuhusu miradi inayotekelezwa na Wizara ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; mfumo wa anwani za makazi; na mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili kila mtumishi aifahamu na kuwa balozi mzuri kwa wananchi.

“Tunatakiwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati, weledi, uadilifu, viwango na ubora unaohitajika na tunapoenda kuitambulisha miradi tunayotekeleza kwa jamii tunatakiwa kuelezea jinsi miradi hiyo inavyoenda kugusa maisha ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”, amefafanua Mhandisi Kundo

Mhandisi Kundo amezungumzia haki na wajibu kwa mtumishi wa umma kuwa vinaenda pamoja na ametoa rai kwa wafanyakazi wa Wizara hiyo wanapodai haki na maslahi yao pia wakumbuke kuwa wanapaswa kuhakikisha wanaitendea haki miradi inayotekelezwa chini ya Wizara hiyo kwa kuwa wafanyakazi hao ndio wanaotengeneza taswira nzuri ya Wizara ambayo ndio atakayoibeba Waziri wao.

“Nasisitiza haki bila kupinda, haki hiyo ishuke mpaka kwenye utekelezaji wa miradi, tuitendee haki miradi yetu kwa kila mfanyakazi kulitendea haki eneo lake kitaalamu kulingana na taaluma yake”, amesisitiza Mhandisi Kundo

Aidha, Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa Menejimenti ya Wizara hiyo kujali na kutengeneza mazingira ya wasaidizi wao kuona fahari katika nafasi zao za kiutumishi na mchango wanaotoa katika utekelezaji wa majukumnu kwa kuwa mafanikio ya Wizara yanajumuisha watumishi wote mpaka ngazi ya wasaidizi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilim ali Watu, Teddy Njau amesema kuwa kikao hicho cha baraza la wafanyakazi kimefanyika kwa siku mbili ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya mwaka wa fedha 2021/22 ambapo kati ya shilingi bilioni 83 zilizoelekezwa kwenye miradi hiyo, tayari shilingi bilioni 76 zimeshatumika hadi mwezi Februari mwaka huu 2022.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE wa Tawi la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Laurencia Masigo amempongeza Naibu Waziri huyo kwa kuendelea kuitangaza Wizara na kuiwakilisha vema kwa wananchi pamoja na wakurugenzi wa Wizara hiyo kwa kuendelea kusimamia miradi ya kitaifa inayotekelezwa chini ya Wizara hiyo

Akitoa salamu zake kwa Naibu Waziri, Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatina amesema kuwa amefurahishwa na mwenendo mzima wa baraza hilo ambalo limetimiza wajibu wake kwa kujadili hoja za baraza la wafanyakazi na sio hoja binafsi

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samwel Nyungwa amesema kuwa maelekezo aliyoyatoa Naibu Waziri huyo yamepokelewa na anaamini wafanyakazi wa Wizara hiyo wanaenda kutekeleza kwa kutafsiri miradi ya maendeleo kwa wananchi, kutambua mipaka yao katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa viwango na muda unaohitajika.