Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Waziri Kairuki Akagua Mradi wa Bilioni 4.5 Mpwapwa , Asisitiza Ubora na Uwajibikaji katika Kukamilisha Mradi


Na Mwandishi Wetu - WMTH DODOMA.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha ujenzi wa jengo jipya la ofisi za halmashauri hiyo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora, akisisitiza kuwa fedha za umma zinapaswa kuonekana kupitia thamani ya kazi inayotekelezwa. 

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, Mhe. Kairuki amesema mradi unakadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 4.5, ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 1.8 zimetumika. Amepongeza usimamizi mzuri wa fedha pamoja na kasi ya utekelezaji wa ujenzi huo, huku akieleza kuwa hatua zilizofikiwa zinaonyesha dhamira ya halmashauri hiyo katika kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora ya kutolea huduma.

Aidha, ameahidi kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwa Serikali Kuu ili halmashauri iendelee kupatiwa fedha kwa wakati, akieleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwezesha huduma nyingi kupatikana katika eneo moja na hivyo kupunguza usumbufu wa wananchi kufuata huduma katika maeneo mbalimbali.

Pia amesema jengo hilo litaimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za serikali, huku ukiongeza morali ya kazi, kuimarisha uratibu wa shughuli za kiutendaji na kuongeza tija katika kuhudumia wananchi.

Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ulianza mwezi Machi, 2025 na unatekelezwa na Kampuni ya Azhar Construction Company Ltd. ukiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya utawala na kuboresha huduma kwa wananchi.