Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Waziri Kairuki: TEHAMA ni Msingi wa Huduma Bora za Afya.


Na Mwandishi Wetu, WMTH Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema kuwa mafanikio ya Sekta ya Afya yanategemea kwa kiwango kikubwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), akisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali unapaswa kwenda sambamba na ujenzi wa vituo na hospitali za kisasa.

Akizungumza wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Kituo cha Afya cha Lailaka, kilichopo Kata ya Sagara, wilayani Kongwa, Mhe. Kairuki alisema kuwa majengo bora ya afya pekee hayatoshi bila kuwepo kwa mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha sekta ya afya inanufaika kikamilifu na mageuzi ya kidijitali.

“Kama Waziri mwenye dhamana ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kusisitiza kuwa maendeleo ya Sekta ya Afya na maendeleo ya TEHAMA yanakwenda sambamba. Jengo zuri la afya linahitaji pia mifumo bora ya kidijitali ili kutoa huduma zenye ufanisi,” alisema.

Alieleza kuwa kuunganishwa kwa kituo hicho na huduma za intaneti kutaiwezesha kutumia mifumo ya kielektroniki ya kuhifadhi kumbukumbu za wagonjwa, kuagiza na kufuatilia dawa, pamoja na huduma za ushauri wa kitabibu kwa njia ya mtandao (telemedicine), zitakazowaunganisha wananchi na madaktari bingwa waliopo katika hospitali za rufaa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Aidha, Waziri Kairuki alisema matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali yataongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kupunguza usumbufu kwa wananchi na kuimarisha uwazi pamoja na uwajibikaji katika usimamizi wa huduma za afya.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA ili kuhakikisha taasisi za afya nchini zinatumia teknolojia kuongeza ubora wa huduma, kupunguza gharama za utoaji wa huduma na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan maeneo ya vijijini.