Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MINARA YENYE KASI YA 5G KUJENGWA ILI KUIFUNGUA LINDI KIUCHUMI


Na Jumaa Wangwe, WHMTH, LINDI 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema minara 54 inajengwa katika Mkoa wa Lindi ili kusaidia shughuli mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huo ikiwemo ile ya mradi mkubwa wa uchimbaji wa gesi.
 
Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Mitwero mkoani Lindi wakati akitoa salamu na kueleza utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara hiyo.
 
“Mheshimiwa Rais katika mikataba ya kupeleka huduma ya mawasiliano vijijini ya minara 758 uliyoshuhudia ikisainiwa Mkoani Dodoma, Mkoa wa Lindi umepata minara 54 ambapo nguvu kubwa itawekezwa katika eneo hili ili kuhakikisha TEHAMA inaifungua Lindi kiuchumi”. amesema Waziri Nape
 
“Kuna baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Lindi mahitaji yamekuwa makubwa na hasa katika eneo hili unapojengwa mradi wa gesi, eneo la hospitali na madini na nimeshaagiza wataalamu kuanzia mwezi ujao watafika kwa ajili ya kuangalia maeneo ya kuweka minara hiyo itakayotoa huduma ya 5G”. Amesema Waziri Nape
 
Rais Dkt. Samia anamalizia ziara yake ya Mikoa ya kusini ambapo alianza na Mkoa wa Mtwara na sasa yupo Mkoani Lindi.