Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MHE. MHA. KUNDO: TANZANIA KUWA KITOVU CHA TEHAMA


Serikali imepanga Tanzania kuwa kitovu cha maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT HUB) Afrika Mashariki kwa kuwa mitandao ya kimataifa (SUB-MARINE CABLES)  imeanzia Tanzania na kugawanyika kwa nchi zingine za Afrika

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Wizara Ya Habari, Mawasiliano Na Teknolojia Ya Habari Mhe. Mha. Kundo Mathew wakati wa kikao cha tathmini ya utendaji kwa Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake kilichofanyika tarehe 26, Julai 2022 katika ukumbi wa Kibo Palace, jijini Arusha

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mha. Kundo amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan imeiamini Wizara hiyo na kuipa jukumu la kuhakikisha inaboresha mifumo ya TEHAMA ili kuendelea kurahisisha huduma za mawasiliano kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla

Aidha, baada ya kikao hicho watumishi wa wizara hiyo wametakiwa kupanga mipango mikakati ya utekelezaji ambao ni wa mwaka 2022/2023, huku ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutekeleza bajeti iliyopitishwa na bunge la Jmamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kutatua baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika utendaji

Vilevile Mhe. Mha. Kundo ameongeza kuwa ili kuendana na mabadiliko ya TEHAMA yanayoendelea duniani ni lazima Serikali kupitia Wizara hiyo ifanye tathimini nzuri ya kujua yanayopaswa kufanyika ili kuboresha miundombinu ya TEHAMA.

“Ili tuhakikishe kwamba Tanzania inakuwa kituo cha ICT HUB ni lazima mipango hii ikakamilishwe kwa weledi kwa sababu ili uende m,bele ni lazima ufanye tathmini ya tunakotoka, tulipo, na hata tunapoelekea”.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa umuhimu wa mkutano huo ni kuainisha mipango, kuleta utofauti katika utendaji kazi,  kutoa dira mpya na kutekeleza sera mbalimbali ya Wizara vilevile kuibua fursa mpya zilizopo katika Wizara na  kuleta ushindani wa kiuchumi dhidi ya nchi nyingine

Katika hatua nyingine akizungumza kwa njia ya simu Waziri wa Habari, Mawasiliano Na Teknolojia Ya Habari Mhe. Nape Nnauye amesisitiza umoja kuwa msingi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo Pamoja na Taasisi zake. Ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuifanya Wizara hiyo kuleta tija kwa taifa na kuenda sambamba na imani ya Rais kwa Wizara hiyo

“Mhe. Rais Samia ametuweka hapa kwa Makusudi na kwa sababu ameamini tutakuwa na mchango kwenye Sekta zetu”.

Pia, amewataka watumishi Taasisi walioko chini ya Wizara hiyo kuwajibika katika nafasi zao na kila mmoja kuhakikisha anaacha alama kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kutoa huduma bora kwa wananchi kulingana na mahitaji yao